17. Radd juu ya utata wa kwamba hakuwezi kutokea shirki katika kisiwa cha kiarabu

Tano: Miongoni mwa shubuha zao ni kutumia kwao dalili kwa Hadiyth isemayo:

“Shaytwaan amekata tamaa ya kuabudiwa katika kisiwa cha kiarabu.”

Ni Hadiyth ambayo imepokelewa kupitia njia nyingi katika “as-Swahiyh” ya Muslim na nyenginezo. Imetumiwa kama dalili juu ya kutokuwezekana kabisa kutokea shirki katika kisiwa cha kiarabu. Jibu juu ya hilo ni kwa yale aliyosema Ibn Rajab (Rahimahu Allaah):

“Kinachokusudiwa ni kwamba amekata tamaa Ummah mzima kukusanyika katika shirki kubwa.”

Ibn Kathiyr vilevile ameashiria maana hii wakati alipokuwa akifasiri maneno Yake (Ta´ala):

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ

“Leo nimekukamilishieni dini yenu.”[1]

Isitoshe kwa mujibu wa Hadiyth yenyewe aliyekata tamaa ni shaytwaan kwa kudhani na kwa kufikiria kwake na si kwamba amefanya hivo kwa ujuzi. Kwa sababu shaytwaan hajui mambo yaliyofichikana. Haya ni mambo yaliyofichikana na hakuna ayajuaye isipokuwa Allaah pekee. Dhana yake hii ni kuzikadhibisha Hadiyth zilizothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambazo ameeleza ndani yake kwamba kutatokea shirki katika Ummah huu baada yake na uhalisia wa mambo vilevile unamkadhibisha. Kwani waarabu wengi wameritadi kutoka katika Uislamu baada ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa aina mbalimbali za kuritadi. Allaah ndiye anajua zaidi.

[1] 05:05

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Haqiyqat-it-Tawhiyd, uk. 29-30
  • Imechapishwa: 28/03/2019