Kisha Shaykh (Rahimahu Allaah) akabainisha kuwa mambo yakafanywa kinyumenyume kwa wengi wanaodai elimu na kwamba wanaofanya hivo ni wale waongofu kabisa katika watu na walinzi wa Shari´ah. Kwa mtazamo wao walii ni yule asiyewafuata Mitume, hapambani katika njia ya Allaah, hamwamini na wala hamchi. Nitakuwa nimefanya jambo jema ikiwa nitanukuu hapa yale aliyoandika Shaykh-ul-Islaam bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake “al-Furqaan bayn Awliyaa´-ir-Rahmaan wa Awliyaa´-ish-Shaytwaan”:

“Amebainisha (Subhaanah) katika kitabu Chake na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba Allaah anao mawalii katika watu kama ambavo shaytwaan pia anao mawalii wake. Ipo tofauti kati ya mawalii wa Allaah na mawalii wa shaytwaan. Amesema (Ta´la):

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ لَهُمُ الْبُشْرَىٰ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۚ لَا تَبْدِيلَ لِكَلِمَاتِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hakuna khofu juu yao na wala hawatohuzunika – wale ambao wameamini na wakawa wanamcha Allaah. Watapata bishara katika uhai wa dunia na wa Aakhirah. Hakuna mabadiliko katika maneno ya Allaah – huko ndiko kufuzu kukuu.”[1]

Pia amewataja mawalii wa shaytwaan. Amesema (Ta´ala):

فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ إِنَّهُ لَيْسَ لَهُ سُلْطَانٌ عَلَى الَّذِينَ آمَنُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ إِنَّمَا سُلْطَانُهُ عَلَى الَّذِينَ يَتَوَلَّوْنَهُ وَالَّذِينَ هُم بِهِ مُشْرِكُونَ

“Unaposoma Qur-aan basi [anza kwa] kuomba ulinzi kwa Allaah dhidi ya shaytwaan aliyefukuzwa mbali. Hakika yeye hana mamlaka juu ya wale walioamini na kwa Mola wao wanatagemea. Hakika mamlaka yake ni juu ya wale wanaomfanya rafiki mwandani na ambao wao wanamshirikisha.”[2]

Kwa hivo ni lazima kutofautisha kati ya hayo makundi mawili kama ambavo Allaah na Mtume wake walivowafarikisha baina yao. Mawalii wa Allaah ni wale wenye kumwamini na wenye kumcha… nao ni wale ambao wamemwamini na wakajenga urafiki Naye, wakapenda yale anayoyapenda, wakachukia yale anayochukia, wakaridhia yale aliyoridhia, wakakasirishwa na yale yaliyomkasirisha, wakaamrisha yale aliyoamrisha, wakakataza yale aliyokataza, wakampa yule ambaye imewajibika kumpa, wakamnyima yule ambaye imewajibika kumnyima… Kwa hivyo hawi walii wa Allaah isipokuwa yule ambaye amemwamini, akaamini yale aliyokuja nayo na akayafuata kwa ndani na kwa nje.

Yule mwenye kudai kumpenda Allaah na kwamba yeye ni walii Wake na asimfuate – bi maana Mtume – basi huyo si katika mawalii wa Allaah. Bali yule anayekwenda kinyume naye basi anakuwa ni miongoni mwa maadui wa Allaah na mawalii wa shaytwaan. Amesema (Ta´ala):

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ

“Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi. Hivyo atakupendeni Allaah.”[3]

Watu ni wenye kutofautiana katika kuchukuliwa kwao ni mawalii wa Allaah kutegemea na kushindana kwao katika imani na uchaji. Vivyo hivyo wanatofautiana katika kuchukuliwa kwao ni maadui wa Allaah kutegemea na kushindana kwao katika ukafiri na unafiki… Mawalii wa Allaah wako katika daraja mbili; waliotangulia na kukurubishwa na watu wa kuliani walio kati na kati. Allaah amewataja maeneo mengi katika Kitabu Chake kitukufu mwanzoni mwa Suurah “al-Waaqi´ah” na mwishoni mwake, katika “al-Insaan”, “al-Mutwaffifiyn” na katika Suurah “at-Twuur”…  Pepo iko na ngazi mbalimbali zenye kushindana sana. Mawalii wa Allaah ni waumini na wenye kumcha wataokuwa katika ngazi hizo kutegemea imani na kumcha kwao Allaah.

Yule ambaye hajikurubishi kwa Allaah kwa njia ya kwamba hafanyi matendo mema na kujiepusha na matendo maovu basi hawi katika mawalii wa Allaah. Haijuzu kwa yeyote kuona kuwa yeye ni walii wa Allaah khaswa ikiwa hoja yake kwamba ni kujua jambo fulani lililofichika lililosikika kutoka kwake au mwenendo aina fulani… Haijuzu kwa yeyote kujengea hoja kwa sababu ya hayo peke yake ya kwamba eti mtu fulani ni walii wa Allaah ingawa hajui kutoka kwake kinachopunguza uwalii wa Allaah. Tusemeje ikitambulika kuwa hufanya mambo yanayopingana na uwalii wa Allaah? Kwa mfano ikitambulika kuwa haamini ulazima wa kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) si kwa ndani wala kwa nje, bali anaamini kuwa yeye anafuata Shari´ah kwa ndani pasi na uhakika wa nje au anaonelea kuwa mawalii wa Allaah wanayo njia ya kuweza kumfikia Allaah isiyokuwa njia ya Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Kujengea juu ya haya yule mwenye kudhihirisha uwalii na wakati huohuo hatekelezi faradhi na wala hajiepushi na maharamisho, bali pengine akafanya mambo yanayopingana na hayo. Basi haifai kwa yeyote kusema kuwa ni walii wa Allaah… Mawalii wa Allaah hawana chochote kinachowapambanua na watu wengine kwa uinje katika mambo yanayoruhusiwa… Si katika sharti ya walii wa Allaah awe amekingwa na makosa na kwamba hakosei. Bali kuna uwezekano akawa hajui na kutatizwa na baadhi ya mambo ya Shari´ah… Ilipokuwa inafaa kwa walii wa Allaah kukosea basi ikawa sio lazima kwa watu kuamini yale yote anayoyasema yule ambaye ni walii wa Allaah ili asifanane na Mtume… bali ni lazima hayo yote yapimwe juu ya yale aliyokuja nayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam); yakiafikiana nayo, basi atakubaliwa, yasipoafikiana nayo, hatokubaliwa. Isipojulikana kama ameafikiana au hakuafikiana naye basi watu watachukua msimamo wa kukomeka juu yake.

[1] 10:62-64

[2] 16:98-100

[3] 03:31

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 28-30
  • Imechapishwa: 27/06/2021