17. Nguzo na sharti za “Laa ilaaha illa Allaah”

Wanachuoni wetu (Rahimahumu Allaah) wamesema kwamba “Laa ilaaha ila Allaah” ina nguzo, sharti zake, haki zake, mambo yake ya wajibu na mambo yenye kuikamilisha.

Nguzo zake ni mbili:

1 – Kukanusha.

2 – Kuthibitisha.

Kukanusha kumechukuliwa kutoka katika sentesi:

“Hapana mungu wa kweli… “

Kuthibitisha kumechukuliwa kutoka katika sentesi:

“… isipokuwa Allaah”.

Maana yake ya kijumla ni kwamba hakuna mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah Mmoja asiyekuwa na mshirika. Kumwabudu Yeye ndio haki na kuwaabudu wengine miongoni mwa masanamu, mizimu na waungu wengineo wanaoabudiwa badala ya Allaah kuabudiwa kwao ni kwa batili. Wataulizwa wale waliotumbukia ndani ya ´ibaadah hizo. Kumwabudu mwengine asiyekuwa Allaah ndio jarima kubwa ulimwenguni na ndio dhambi kubwa aliyoasiwa kwayo Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Dalili ni kwamba Allaah hamsamehi mwenye nayo akifa juu yake. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoulizwa: “Ni dhambi ipi kubwa?” Akasema:

“Kumfanyia Allaah mshirika ilihali Yeye ndiye kakuumba.”[2]

Kama walivyolitajia nguzo zake wamelitaja vilevile kwamba lina sharti saba baada ya kufanya tafiti za kielimu na kufuatilia ndani ya Qur-aan na Sunnah.

1- Sharti ya kwanza: Elimu ya kujua maana yake. Hayo ni kwa sababu pindi mja anapotamka shahaadah ni lazima ajue maana yake. Kwa msemo mwingine maana yake ni hakuna mwabudiwa mwengine wa haki isipokuwa Allaah. Kila sharti miongoni mwa masharti yake ina kinyume chake. Kinyume cha elimu ni ujinga. Hayo ni kwa sababu yule mwenye kujahili maana yake hawezi kutendea kazi ile elimu inayofahamishwa nalo mpaka kwanza ajue maana yake. Hiyo ndio sababu iliyomfanya al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) kusema:

“Mlango: Elimu kabla ya kauli na kitendo.”

Kwa sababu pia ndio msingi wa dini ni lazima kwa kila muislamu wa kiume na wa kike ajifunze nguzo na sharti za shahaadah ijapo kwa njia ya wazi iliojumla.

2 – Sharti ya pili: Yakini. Hayo ni kwamba yule mwenye kutamka shahaadah anatakiwa awe mwenye kuyakinisha ile inayofahamishwa nalo, ambayo ni kukanusha na kuthibitisha. Kinyume chake ni shaka. Haijuzu kwa muislamu kutilia shaka ile maana yenye kufahamishwa na shahaadah.

3 – Sharti ya tatu: Kukubali yale yanayofahamishwa nalo katika maana tukufu ambayo ni kule kukanusha na kuthibitisha. Kwa msemo mwingine ni kwamba mtu anatakiwa kuyakubali hayo kwa moyo mkunjufu, moyo wenye utulivu na imani yenye kina kwamba yale yanayofahamishwa na neno hili ndio asili na msingi wa dini. Kinyume chake ni kulikataa, jambo ambalo limefanywa na makafiri wa Quraysh ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaelekezea Da´wah. Matokeo yake wakamkatalia neno hili kwa ajili ya kung´ang´ania kuabudu masanamu na mizimu waliyowakuta mababa na mababu. Kukatokea vita na Allaah (´Azza wa Jall) akawanusuru kundi la waumini lililokuwa likiongozwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) dhidi ya wale makafiri wapuuzi ambao hawakujisalimisha kwenye neno la Ikhlaasw isipokuwa baada ya mivutano na maudhi mengi waliyomfanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kundi la waumini lililokuwa dogo ambalo lilimfuata pale mwanzonimwanzoni. Miongoni mwao wako waliohama kwenda Uhabeshi na wengine wakabaki wakiwa ni wenye kujificha mpaka pale Allaah (´Azza wa Jall) alipowaletea ushindi wa wazi. Mpaka ilipofikia kuhajiri na kufunguliwa mji wa Makkah ambapo watu waliingia ndani ya dini ya Allaah makundi kwa makundi. Haki ikashinda, neno hili likawa juu ambalo kwa ajili yake ndio Allaah amewaumba watu na majini, mbingu na ardhi, Pepo na Moto, kukawekwa Shari´ah ya jihaad, Da´wah, nasaha, kuamrishana mema na kukatazana maovu. Yote hayo kwa ajili ya kuhakikisha maana ya neno hili tukufu “Laa ilaaha illa Allaah”.

4 – Sharti ya nne: Unyenyekevu. Mtu anatakiwa kunyenyekea na kujisalimisha kwa nje na kwa ndani kwa ile maana iliyofahamishwa na neno hili la Ikhlaasw. Kinyume chake ni kuacha.

5 – Sharti ya tano: Ukweli. Kulisadikisha. Maana yake ni kwamba ukisema “hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah” ni lazima uwe mkweli kwa yale unayoyasema kwa nje na kwa ndani. Dalili ya kulifanyia ukweli ni wewe kumpwekesha Mola Wako kwa ´ibaadah zote za kimali, za kimwili au zote mbili ambaye yupeke yake hana mshirika. Usimwelekezee mwengine ´ibaadah isipokuwa Yeye tu. Hivo ndivo alivyokuamrisha Allaah (´Azza wa Jall) pale aliposema:

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako ameamuru kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye pekee.”[3]

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe Yeye na chochote.”[4]

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[5]

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote yule anayeomba pamoja na Allaah mungu mwengine – hana ushahidi wa wazi juu ya hilo – basi hakika hesabu yake iko kwa Mola wake. Hakika hawafaulu makafiri.”[6]

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ ۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini kwa kujiengua na shirki na kuelemea Tawhiyd na wasimamishe swalah na watoe zakaah – na hiyo ndiyo dini iliyosimama imara.”[7]

Yapo maandiko mengine ambayo Allaah (´Azza wa Jall) amewaamrisha wale ambao ´ibaadah ni yenye kuwalazimu kumwelekezea Yeye ´ibaadah zao katika kutekeleza maamrisho, kujiepusha na makatazo, kuhalalisha ya halali, kuharamisha ya haramu, kutekeleza faradhi, kusimamisha adhabu za Kishari´ah, kutekeleza mambo ya wajibu na kujikurubisha kwa Allaah kwa yale mambo yaliyopendekezwa. Hizi ndio ´ibaadah ambazo Allaah amewalazimu kwazo viumbe wote katika walimwengu wa kiwatu na wakijini.

Kwa hivyo maana ya ukweli anatakiwa awe mkweli na mwenye kusadikisha kwa yale yanayofahamishwa na neno hili kubwa katika maana yake. Kinyume cha ukweli ni uongo kama walivofanya makafiri wa Quraysh na wale waliofuata mkondo wao katika kipindi cha Mtume mtukufu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wafuasi wao mpaka siku ya Qiyaamah. Ni jambo ambalo limepingwa na waabudia mizimu, waabudia makaburi, wale wenye kupetuka mipaka kwa waja wema na wakanamungu ambao hawaamini uwepo wa Allaah, Pepo, Moto, kufufuliwa na kukusanywa. Mayahudi pia wamekadhibisha. Wakristo pia wamekadhibisha. Matokeo yake Allaah akawakasirikia hao wote kwa sababu hawakusadikisha neno hili, bali wamemfanyia Allaah mungu mwengine.

Mkafiri wenye kuabudia masanamu wamemfanyia Allaah waungu wengine katika miti, mawe, masanamu na makaburi ambayo wanayatekelezea nadhiri na vichinjwa. Pia wanawataka msaada wale waliyomo ndani yake ambao wanawaita kuwa ni “mawalii” katika kuleta manufaa na kuzuia madhara. Matokeo yake wakakhasirika. Mayahudi wameabudu imani ya utatu na vivyo hivyo wakristo. Allaah (´Azza wa Jall) amebainisha katika maneno Yake:

وَقَالَتِ الْيَهُودُ عُزَيْرٌ ابْنُ اللَّـهِ وَقَالَتِ النَّصَارَى الْمَسِيحُ ابْنُ اللَّـهِ

”Mayahudi wanasema ”‘Uzayr ni mwana wa Allaah”.”

Wamemfanyia Allaah mtoto.

وَقَالَتِ الْيَهُودُ عُزَيْرٌ ابْنُ اللَّـهِ وَقَالَتِ النَّصَارَى الْمَسِيحُ ابْنُ اللَّـهِ

”Mayahudi wanasema ”‘Uzayr ni mwana wa Allaah”.”[8]

Allaah akawaraddi na akawasema vibaya:

ذَٰلِكَ قَوْلُهُم بِأَفْوَاهِهِمْ ۖ يُضَاهِئُونَ قَوْلَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَبْلُ ۚ قَاتَلَهُمُ اللَّـهُ ۚ أَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ

“Hiyo ni kauli yao kwa midomo yao. Wanayaiga maneno ya wale waliokufuru kabla. Allaah awaangamize! Ni vipi wanageuzwa?”[9]

Amesema vibaya pia kwa kusema:

اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ

“Wamewafanya marabi wao na watawa wao kuwa ni waungu badala ya Allaah na al-Masiyh, mwana wa Maryam.”[10]

Bi maana wamewafanya wanazuoni na watawala kuwa ni waungu. Wanawahalalishia yaliyo ya haramu na hivyo wakawafuata katika hayo na wanawaharamishia yaliyo ya halali na wakawafauta katika hayo. Ndipo Allaah (´Azza wa Jall) akawasema vibaya kwelikweli ili Ummah wa Qur-aan uweze kupata mazingatio na mawaidha kutokana na matendo yao ambayo Allaah ameyaweka wazi pale aliposema:

اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ سُبْحَانَهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ

“Wamewafanya marabi wao na watawa wao kuwa ni waungu badala ya Allaah na al-Masiyh, mwana wa Maryam, ilihali hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Mungu Mmoja pekee. Hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye. Utakasifu ni Wake kutokamana na yale yote wanayomshirikisha nayo.”[11]

Kuhusu wakanamungu miongoni mwa wale wanaoamini mazingira kwa aina zao mbalimbali hawaamini uwepo wa Allaah (´Azza wa Jall). Wanaamini kuwa mazingira yenyewe ndio yanaendesha ulimwengu. Wanapoulizwa kuhusu mazingira hayo wanasema kuwa ni nguvu yenye kutenda ilihali ukweli wa mambo hawajui uhakika wake, jambo ambalo ni ukafiri wenye upeo wa juu.

6 – Sharti ya sita: Ikhlaasw. Kinyume chake ni shirki. Matendo ya mshirikina ni batili na ni yenye kurudishwa kwake mwenyewe. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَقَدِمْنَا إِلَىٰ مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاءً مَّنثُورًا

”Tutayaendea yale waliyoyatenda katika matendo, Tutayafanya kuwa ni vumbi lililotawanyika.”[12]

7 – Sharti ya saba: Mapenzi kulipenda neno hili na kupenda ile maana yenye kufahamishwa nalo. Vilevile kumpenda yule Aliyeliteremsha na ameamrisha lihakikiwe kwa nje na kwa ndani na wale wenye kulingania kwalo katika Mitume na Manabii na wale waliorithi elimu na Da´wah yao. Kwa hivyo yule mwenye kulipenda, akampenda Aliyeliamrisha na akapenda ile maana iliyofahamishwa nalo ndiye muislamu wa kweli. Na yule mwenye kulichukia na akamchukia aliyekuja nalo na asitendee kazi ile maana iliyofahamishwa nalo, mtu kama huyo hana lolote kuhusiana na Uislamu. Kinyume cha mapenzi ni kuchukia.

8 – Sharti ya nane: Kukufuru vile vyenye kuabudiwa badala ya Allaah. Kwa hivyo hakuna kupenda isipokuwa kwa kujitenga mbali. Kwa msemo mwingine haipatikani uhakika wake mpaka Tawhiyd imeambatana na kujitenga mbali na shirki na washirikina. Tunazirudi sharti hizi saba kwa njia ya ujumla ili mtu aweze kuzihifadhi:

1 – Elimu.

2 – Yakini.

3 – Kuikubali.

4 – Kulinyenyekea.

5 – Ukweli.

6 – Ikhlaasw.

7 – Mapenzi.

8 – Kukufuru vile vinavyoabudiwa badala ya Allaah.

Kuhusu haki zake na mambo yenye kulikamilisha ni yale mambo mengine yote ya ´ibaadah ya Kishari´ah katika faradhi, mambo ya wajibu ambayo Allaah ameamrisha kuyafanya, kutendea kazi muqtadha yake, kujiepusha na mambo ya haramu na kufanya yale mambo yaliyopendekezwa. Yote haya ni mambo yenye kuikamilisha “Laa ilaaha illa Allaah” na yanamtolea ushahidi mwenye nayo kuwa ni mkweli na ni kuyapenda.

[1] 04:48

[2] al-Bukhaariy (04/266) na Muslim (01/90).

[3] 17:23

[4] 04:36

[5] 72:18

[6] 23:117

[7] 98:05

[8] 09:30

[9] 09:30

[10] 09:31

[11] 09:31

[12] 25:23

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Twariyqal-Usuwl ilaa idhwaah-ith-Thalaat-il-Usuwl, uk. 35-41
  • Imechapishwa: 25/11/2021