Swali 17: Je, ni lazima kwa waislamu wote ulimwenguni kufunga kwa muonekano mmoja? Vipi watafunga waislamu wanaoishi katika baadhi ya miji ya kikafiri ambayo haina muonekano kwa mujibu wa Shari´ah?

Jibu: Wanachuoni wametofautiana juu ya masuala haya. Ukionekana mwezi katika mji miongoni mwa miji ya waislamu na ukathibiti maono kwa mujibu wa Shari´ah ni lazima kwa waislamu waliobaki kutenda kazi kwa mujibu wa maono haya? Miongoni mwa wanachuoni wako waliosema kuwa itawalazimu kutenda kazi kwa mujibu wa mwezi huu. Wamejenga dalili kwa ueneaji wa maneno Yake (Ta´ala):

فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi mpya na afunge na atakayekuwa mgonjwa au safarini, basi atimize idadi katika masiku mengine..”[1]

Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mkiuona, basi fungeni.”

Wamesema kuwa hapa wanazungumzishwa waislamu wote. Miongoni mwa mambo yanayotambulika ni kuwa hakukusudiwi kwamba kila mtu auone mwezi kwa nafsi yake mwenyewe, hicho ni kitu kisichowezekana. Kinachokusudiwa ni kwamba wakiuona wale ambao wanazingatiwa kuingia kwa mwezi, jambo ambalo ni lenye kuenea kila mahali.

Wanachuoni wengine wakaona kuwa ikiwa yanatofautiana machomozo ya mwezi, basi kila mahali wana maono yao. Ikiwa hayatofautiani machomozo ya mwezi basi inawalazimu wale ambao hawakuona mwezi kuafikiana na kutenda kazi kwa mujibu wa maono haya muda kuwa mwezi umethibiti kuonekana katika nchi ambayo wanaafikiana katika machomozo yao. Wamejengea hoja kwa yale waliyojengea hoja wale wa mwanzo. Wamesema kuwa Allaah (Ta´ala) amesema:

فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ

“Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi mpya na afunge.”

Miongoni mwa mambo yanayotambulika ni kwamba hakukusudiwi kila mmoja auone kivyake. Basi mwezi huu utatendewa kazi katika yale maeneo ulipoonekana na katika kila maeneo ambayo yanaafikiana na machomozo ya mwezi mwandamo. Kuhusu wale ambao hawaafikiani nao katika machomozo ya mwezi mwandamo, basi hawakuuona kihakika wala kihukumu. Wamesema kwamba vilevile wanasema juu ya maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mkiuona, basi fungeni, na mkiuona fungueni.”[2]

Ambaye yuko maeneo ambayo hayaafikiani na maeneo ya yule muonaji katika machomozo ya mwezi mwandamo anazingatiwa hakuuona si kihakika wala kihukumu. Wamesema kuwa nyakati za mwezi ni kama nyakati za kila siku. Kama ambavo miji inatofautiana katika kujizuia na kufungua swawm kwa kila siku, vivyo hivyo wanalazimika watofautiane katika kujizuia na kufungua kwa mwezi. Ni jambo linalojulikana kuwa kutofautiana kwa kila siku kuna athari zake kwa maafikiano ya waislamu. Walioko mashariki wanajizuia kabla ya wale walioko magharibi na pia wanafungua swawm kabla yao. Tukihukumu kutofautiana kwa machomozo ya mwezi katika nyakati za kila siku basi ni vivyo hivyo katika nyakati za mwezi. Mtu hawezi kusema juu ya maneno Yake (Ta´ala):

فَالْآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُوا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ ۚ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ

“Basi sasa changanyikeni nao [waingilieni] na tafuteni Aliyokuandikieni Allaah kwenu. Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni swawm mpaka usiku.”[3]

kuhusu maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Usiku ukija hapa [mashariki] na ukaondoka mchana hapa [magharibi] na likazama jua, basi amekwishafungua mfungaji.”[4]

Hakuna yeyote anaweza kusema kwamba haya ni yenye kuwaenea waislamu ulimwenguni mzima. Kadhalika tunasema juu ya ueneaji wa maneno Yake (Ta´ala):

فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ

“Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi mpya na afunge.”

Vilevile maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mkiuona, basi fungeni, na mkiuona fungueni.”[5]

Maoni haya, kama unavyoona mwenyewe, yana nguvu kwa mujibu wa matamshi, mtazamo sahihi na pia kipimo sahihi; kipimo cha nyakati za mwezi juu ya nyakati za kila siku.

Wanachuoni wengine wakaona kuwa jambo hili limefungamana na watawala katika masuala haya. Pale ambapo wataona ulazima wa kufunga hali ya kutegemea mashiko ya Shari´ah, basi itawalazimu watu kutenda kwa muqtadha yake. Lengo ni ili watu wasitofautiane na kufarikiana chini ya uongozi mmoja. Watu hawa wamejenga hoja kwa ueneaji wa Hadiyth:

”Fungeni siku mnaanza kufunga na fungueni siku mnapofungua.”[6]

Yapo maoni mengine yaliyotajwa na wanachuoni wanaonakili tofauti katika masuala haya.

Kuhusu kipengele cha pili cha swali kinachouliza ni namna gani watafunga waislamu wanaoishi katika baadhi ya miji ya kikafiri ambayo haina muonekano kwa mujibu wa Shari´ah. Watu hawa wanaweza kuona mwezi mwandamo kwa njia ya Shari´ah kwa wao kuutafuta mwezi wakiweza kufanya hivo. Wasipoweza kufanya hivo, ikiwa tutachagua maoni ya mwanzo juu ya masuala haya basi watalazimika kutenda kwa mujibu wa maono ya nchi ya Kiislamu ambayo kumethibiti kuonekana kwa mwezi mwandamo. Ni mamoja wao wameuona au hawakuuona. Tukichagua maoni ya pili ambapo kila nchi kujitegemea ikiwa machomozo yake yanatofautiana na nchi nyingine katika machomozo ya mwezi na wakati huohuo wakashindwa kuhakiki maono katika nchi aliyomo, basi watazingatiwa nchi iliokaribu zaidi na wao. Kwa sababu hili ndio kubwa wawezalo kulifanya.

[1] 02:185

[2] al-Bukhaariy (1900) na Muslim (2471).

[3] 02:187

[4] al-Bukhaariy (1954) na Muslim (2526).

[5] al-Bukhaariy (1900) na Muslim (2471).

[6] at-Tirmidhiy (697). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 48 mas-alatu fiy Swiyaam, uk. 18-21
  • Imechapishwa: 16/04/2021