17. Mwenye busara na hisia za watu


1- Ni wajibu kwa aliye na busara ajipendekeze kwa watu kwa kuwa na tabia njema na kuacha tabia mbaya. Tabia njema inafuta madhambi kama ambavyo jua linayayuka kwenye barafu. Tabia mbaya inaharibu matendo kama jinsi siki inaharibu asali. Mtu anaweza kuwa na tabia njema nyingi na tabia mbaya moja na tabia mbaya moja hii ikaharibu zile tabia njema zote.

2- Ibn ´Abbaas amesema:

“Kizazi kinakatwa na neema zinakanushwa. Sijaona kitu kama mioyo kukurubiana.”

3- al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw amesema:

“Ukitangamana basi tangamana na mtu aliye na tabia njema. Haiti isipokuwa katika kheri. Kutangamana naye ni raha. Usitangamane na mtu aliye na tabia mbaya. Haiti isipokuwa katika shari. Kutangamana naye ni maumivu. Napendelea zaidi kutangamana na mtenda dhambi aliye na tabia njema kuliko mwanachuoni aliye na tabia mbovu. Mtenda dhambi akiwa na tabia njema, huishi kati ya watu kwa akili yake. Atakuwa ni mwepesi kwa watu na watampenda. Mtu wa ´ibaadah akiwa na tabia mbaya watu wataona kuwa ni mwenye kuchosha na hivyo kumchukia.”

4- Hammaad bin Salamah amesema:

“Kuswawm kwenye bustani ni upetukaji.”[1]

 5- Tabia njema inafanya mtu kupendwa. Tabia mbaya inafanya mtu kuchukiwa. Aliye na tabia njema anaichunga heshima yake. Aliye na tabia mbaya anaiharibu heshima yake.”

6- az-Zuhriy amesema:

“Kuna faida yoyote kwa mtu aliye na tabia mbaya?”

7- Maymuun bin Mahraan amesema:

“Kujipendekeza kwa watu ni nusu ya akili. Kuuliza swali kwa njia nzuri ni nusu ya elimu. Kuishi maisha mepesi ina maana kuwa unahitaji kufanya kazi kidogo kama kawaida.”

8- Ni bora kuwahitaji watu na wakampenda kuliko kutowahitaji na wakamchukia. Kinachowazuia kutompenda mtu ni tabia mbaya. Mtu aliye na tabia mbaya anaichosha familia yake na majirani wake na ni mzigo kwa ndugu zake. Hapa ndipo hutaka kujikwamua naye na kumuombea kufa.

9- Watu wanamweleza mtu mchoshaji kwa sababu mbili:

Ya kwanza: Anafanya yale aliyoharamisha Allaah. Mwenye kuvuka mipaka ya Allaah anachukiwa na Allaah. Anayechukiwa na Allaah huchukiwa na Malaika. Baada ya hapo huchukiwa ardhini. Kisha unakaribia kutomwona yeyote isipokuwa anamwona kama ni mchoshaji na anamchukia.

Ya pili: Anafanya yale watu wanayochukia. Akiwa namna hiyo watu wanastahiki kabisa kumwona kuwa ni mchoshaji.

10- Abu Mishar ameeleza kuwa Hishaam bin Yahyaa amesema:

“Kwenye pete ya baba yako – Abu Abiy Mishar – kulikuwa kumechongwa “Unachosha! Nenda zako!” Kila wakati mtu alipokuwa akikaa karibu naye na kuona kuwa anachosha anaigeuza pete yake na kumwambia: “Soma kilichoandikwa kwenye pete!” Mtu huyo akishasoma anaenda zake.”

[1] ”Bi maana kufunga swawm za Sunnah pindi mtu ametoka na marafiki zake na kutembea kwenye mabustani ambapo kuna matunda ambayo mtu huyapata nadra. Anayefunga katika hali kama hii ni upetukaji.” ”Maelezo ya chini ya ”Rawdhwat-ul-´Uqalaa´”, uk. 65)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 63-67
  • Imechapishwa: 06/02/2018