Swali 17: Mimi ni daktari ambaye nilitumwa nje ya nchi kwa ajili ya kukamilisha masomo yangu. Lakini mke wangu amenitia hatiani kwa sababu ni nchi ya kikafiri na kuniuliza atawezaje kuhifadhi Hijaab. Je, kuonyesha uso ni jambo la haramu khaswa ukizingatia kwamba ndio msingi wa kuingia ndani ya kila nchi?

Jibu: Ni wajibu kwa muumini wa kike kujisitiri na kuvaa Hijaab. Kwani kuonyesha uso wake au kitu katika mwili wake ni fitina. Amesema (Ta´ala) ndani ya Kitabu Chake kitukufu:

وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ ۚ ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ

“Mnapowauliza [wake zake] haja yoyote, basi waulizeni nyuma ya pazia. Hivyo ni utwaharifu zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao.”[1]

Amebainisha (Subhaanah) kwamba Hijaab ni utwaharifu zaidi juu ya mioyo na kutovaa Hijaab ni jambo la khatari juu ya mioyo ya watu wote. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ

“Ee Nabii! Waambie wake zako na mabinti zako – na wanawake [wote] wa Waumini – ya kwamba [nje ya nyumbani] wajiteremshie mavazi yao ya juu; hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane [kuwa ni wanawake wa heshima] na wasiudhiwe.”[2]

Jilbaab ni ile ambayo mwanamke anaiweka juu ya kichwa chake na mwili wake na inamfunika uso wake na mwili wake wote. Inakuwa ni kama ziada juu ya mavazi yake ya kawaida. Amesema (Subhaanah):

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ ۖ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ

“Na waambie waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika; hivyo waangushe khimari zao mpaka vifuani mwao. Na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, baba zao, baba za waume wao, wana wao wa kiume, wana wa kiume wa waume zao, kaka zao, wana wa kiume wa kaka zao, wana wa kiume wa dada zao, wanawake wao [dada zao wa Kiislamu], wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, watumishi wanaume wasio na matamanio [tena kwa wanawake], au watoto ambao [bado] hawaelewi [kitu kuhusu] yanayohusu uke. Na wala wasipige miguu yao [wanapotembea] yajulikane yale wanayoyaficha katika mapambo yao.” [3]

Ni wajibu kwa mwanamke kufunika uso na viungo vyengine vyote mbele ya mwanaume ajinabi. Huyo ni yule mwanaume ambaye sio Mahram yake. Hayo ni kutokana na kuenea kwa Aayah zilizotajwa. Jengine ni fitina na ni miongoni mwa mapambo yaliyo wazi zaidi. Lakini hapana kizuizi akavaa Niqaab ambayo ni ile yenye kuachia jicho moja au mbili pekee. Ikiwa unajisitiri na kuvaa Hijaab mbele ya muumini, basi itakuwa ni aula zaidi kufanya hivo mbele ya kafiri. Haijalishi kitu japo watapinga hilo. Ni kweli wanaweza kufanya hivo lakini baadaye wakalitambua baada ya kuwabainishia kwamba hii ndio Shari´ah ya Uislamu.

[1] 33:53

[2] 33:59

[3] 24:31

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Mariydhw, uk. 39-41
  • Imechapishwa: 03/08/2019