17. Miongoni mwa mambo ambayo mfungaji anapaswa kujiepusha nayo

1- Maneno ya upuuzi, ujinga na maneno ya uongo. Ni haramu kwa mwenye kufunga kuzungumza maneno ya upuuzi ambayo ni yale maneno machafu na vile vitangulizi vya jimaa, ugomvi, ujinga, maneno ya uongo na kuyatendea kazi na matusi. Akimtukana mtu au kupambana naye basi amweleze kuwa amefunga. Asimkabili kwa mfano wake. Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swawm ni ngao. Mmoja wenu akifunga asiseme maneno ya upuuzi na wala asigombane. Mtu akimtukana au kupambana naye, basi aseme: “Nimefunga.”[1]

Katika upokezi mwingine wa al-Bukhaariy kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swawm ni ngao. [Mfungaji] asiseme maneno ya upuuzi wala asifanye ujinga. Mtu akipambana naye au akamtusi, basi aseme: “Nimefunga.”[2]

Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyeeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule asiyeacha maneno ya uongo, kuyatendea kazi na ujinga, basi Allaah hana haja kwa yeye kuacha chakula na kinywaji chake.”[3]

2- Mfungaji hatakiwi kupandisha maji puani sana kwa kuchelea asije kunywa maji kwa kuingia kooni mwake. Hayo ni kutokana na yale waliyopokea waandishi wa “as-Sunan” na yakasahihishwa na Ibn Khuzaymah kupitia kwa Luqaytw aliyesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia:

“Fanya kishindo katika kupalizia isipokuwa kama utakuwa umefunga.”[4]

3- Bora mtu aache kutumia zile dawa za kuweka puani ili zisije kuingia kooni mwake. Kwa sababu pua ni njia inayopitisha chakula.

Kuhusu matone kwenye macho na kwenye masikio na vivyo hivyo kupaka wanja kwenye macho, mfungaji kuchelewesha kuvitumia hivo mpaka wakati wa usiku ndio bora zaidi kwa sababu ya kutoka nje ya tofauti kwa sababu wapo wanachuoni wenye kuyakataza hayo. Ijapokuwa maoni ya sawa ni kwamba havifunguzi kwa kutokuwepo dalili zinazofahamisha hivo. Lakini bora mtu aache kufanya hivo kwa sababu ya usalama zaidi juu ya ´ibaadah hii tukufu.

[1] al-Bukhaariy (1904) na Muslim (1151).

[2] al-Bukhaariy (1894).

[3] al-Bukhaariy (1903).

[4] Abu Daawuud (142) na at-Tirmidhiy (788) na wengineo. at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswaru fiy Ahkaam-is-Swiyaam, uk. 29-31
  • Imechapishwa: 23/05/2019