17. Mgonjwa anaswali ndani ya wakati vile awezavyo

Swali 17: Wagonjwa wengi wanachukulia wepesi jambo la swalah na wanasema kuwa watalipa swalah pale ambapo watapona. Baadhi ya wengine wanahoji kwa kusema ni vipi wataswali ilihali hawawezi kujitwahirisha wala kujiepusha na najisi. Ni zipi nasaha zako kwa watu hawa?

Jibu: Maradhi hayamzuilii mtu kuswali kwa hoja ya kushindwa kujitwahirisha muda wa kuwa akili bado zikingali. Bali ni lazima kwa mgonjwa kuswali kwa kiasi cha uwezo wake na kujitwahirisha kwa maji akiweza kufanya hivo. Asipoweza kutumia maji basi atafanya Tayammum na kuswali. Ni lazima kusafisha najisi kuondoka mwilini mwake na kwenye nguo zake wakati wa kuswali. Vilevile anaweza kuzibadilisha nguo najisi kwa nguo ambazo ni safi wakati wa kuswali. Akishindwa kuosha najisi na kubadilisha nguo ambazo ni najisi kwa nguo ambazo ni safi, basi jambo hilo litadondoka kutoka kwake na ataswali vile ilivyo hali yake. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Mcheni Allaah muwezavyo.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nikikuamrisheni jambo basi lifanyeni muwezavyo.”

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia ´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anhumaa) wakati alipomshtakia maradhi yake akasema:

“Swali kwa kusimama. Usipoweza, kwa kukaa. Usipoweza, kwa kulalia ubavu.”

Ameipokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake.

an-Nasaa´iy ameipokea kwa cheni ya wapokezi Swahiyh na ameongeza:

“Swali, kwa kusimama. Usipoweza, kwa kukaa. Usipoweza, kwa kulalia ubavu. Usipoweza, kifudifudi.”

[1] 64:16

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 20
  • Imechapishwa: 16/08/2022