17. Mapote ya Murji-ah na mtazamo wao juu ya imani

Pamoja na haya Murji-ah wamegawanyika makundi mane:

1- Murji-ah al-Fuqahaa´: Miongoni mwa watu wa Kuufah na Ahnaaf ambao wanasema kuwa imani ni kutamka kwa mdomo na kuamini ndani ya moyo na matendo hayaingii.

2- Ashaa´irah na wale waliofuata madhehebu yao: Wanasema kuwa imani ni kusadikisha kwa moyo ijapokuwa mtu hakutamka kwa mdomo. Ambaye atasadikisha kwa moyo ni muumini hata kama hakutamka. Kujengea juu ya haya makafiri ni waumini. Kwa sababu wanaamini kwa mioyo yao lakini hawatamki kwa midomo yao. Amesema (Ta´ala):

قَدْ نَعْلَمُ إِنَّهُ لَيَحْزُنُكَ الَّذِي يَقُولُونَ ۖ فَإِنَّهُمْ لَا يُكَذِّبُونَكَ وَلَـٰكِنَّ الظَّالِمِينَ بِآيَاتِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ

“Hakika tunajua kwamba yanakuhuzunisha yale wanayoyasema. Hakika wao hawakukadhibishi wewe lakini madhalimu wanakanusha alama za Allaah.”[1]

Walikuwa wakisadikisha kwa mioyo yao na wakitambua kuwa ni Mtume wa Allaah, kwamba Qur-aan ni maneno ya Allaah na kwamba aliyokuja nayo ndio haki. Lakini vizuizi mbalimbali vinawazuia; ima kwa sababu ya kiburi na uzito, kuchelea juu ya nafasi na uongozi wao au hasadi.

Pia mayahudi wanamjua:

الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَعْرِفُونَهُ

“Wale ambao tumewapa Kitabu wanamjua… “

Bi maana Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمْ

“… kama wanavyowajua watoto wao.”[2]

Wanajua kuwa ni Mtume wa Allaah. Lakini hawakumtii na wala hawakuamini ujumbe wake:

حَسَدًا مِّنْ عِندِ أَنفُسِهِم مِّن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمُ الْحَقُّ

“… husuda iliyomo katika nafsi zao; baada ya kuwabainikia kwao haki.”[3]

Waliachana naye kwa sababu ya hasadi. Wanachotaka ni utume uwe kwa wana wa israaiyl na usiwe kwa wana wa ismaa´iyl. Waliwahusudu wana wa israaiyl na ndio maana wakakataa kumwamini Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hiyo walikuwa wakiamini kwa mioyo yao ya kwamba ni Mtume wa Allaah. Hapa kuna Radd kwa Ashaa´irah wanaosema kuwa imani ni kusadikisha kwa moyo ijapkuwa mtu hakutamka kwa mdomo.

3- Karaamiyyah: Wanasema kuwa imani ni kutamka kwa moyo ijapokuwa mtu hakuamini kwa moyo. Mtu akitamka kwa mdomo na akashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah ni muumini hata kama hakuamini ndani ya moyo wake. Hivi ndivo wanavosema, jambo ambalo ni batili. Jambo hili linapelekea kwamba wanafiki ni waumini. Kwa sababu wanasema kwa ndimi zao yasiyokuwemo ndani ya mioyo yao. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ فِي الدَّرْكِ الْأَسْفَلِ مِنَ النَّارِ وَلَن تَجِدَ لَهُمْ نَصِيرًا

“Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka la chini kabisa katika Moto na wala hutompata kwa ajili yao mwenye kunusuru.”[4]

Wao hutamka kwa ndimi zao lakini hawaamini kwa mioyo yao:

إِذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ اتَّخَذُوا أَيْمَانَهُمْ جُنَّةً فَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ

”Watakapokujia wanafiki wakisema: “Tunashuhudia kwamba wewe bila shaka ni Mtume wa Allaah.” – na Allaah anajua vyema kuwa hakika wewe ni Mtume Wake na Allaah anashuhudia kuwa hakika wanafiki bila shaka ni waongo. Wamefanya viapo vyao [vya uongo] kuwa ni kinga wakazuia watu na njia ya Allaah.”[5]

Ushuhuda wao pamoja na Mtume ni kwa sababu tu ya kutaka kujikinga kutokamana na kuuliwa. Wanachotaka ni kuishi pamoja na waislamu ilihali ni makafiri ndani ya nafsi na mioyo yao. Allaah akawahukumu kwamba wako katika tabaka ya chini kabisa Motoni chini ya waabudu masanamu. Licha ya hayo Karraamiyyah wanasema kuwa ni waislamu na ni waumini.

4- Jahmiyyah – nalo ndio pote baya kabisa – ambao wanasema kuwa imani ni kutambua kwa moyo ijapo mtu hakusadikisha. Mtu akitambua kwa moyo wake ni muumini japo hakusadikisha, hakutamka wala hakutenda. Midhali ametambua kwa moyo wake ni muumini. Haya ndio maoni mabaya zaidi ya Murji-ah.

[1] 06:33

[2][2] 02:146

[3] 02:109

[4] 04:145

[5] 63:01-02

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 35-37
  • Imechapishwa: 09/03/2021