17. Kafara kwa yule mwenye kumwingilia mwenye hedhi

15- Kafara ya mwenye kumwingilia mwenye hedhi

Mwenye kumwingilia mwenye hedhi kabla ya kutwaharika kutoka katika hedhi yake, basi ni wajibu kwake kutoa swadaqah ya thamani ya uzito wa dinari ya dhahabu au nusu yake. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya ´Abdullaah bin ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu yule mwenye kumwingilia mkewe ilihali yuko na hedhi ifuatavyo:

“Anatakiwa kutoa dinari moja au nusu ya dinari.”[1]

[1] Wameipokea waandishi wa “as-Sunan”, at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Kabiyr” (01/14/03), (01/146) na (02/148), Ibn-ul-A´rabiy katika “al-Mu´jam” yake (01/15) na (01/49), ad-Daarimiy, al-Haakim, al-Bayhaqiy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh yaliyo juu ya masharti ya al-Bukhaariy. Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim na adh-Dhahabiy, Ibn Daqiyq al-´Iyd, Ibn Turkmaaniy, Ibn-ul-Qayyim, Ibn Hajar al-´Asqalaaniy wakaafikiana naye kama ilivyo katika “Swahiyh Sunan Abiy Daawuud (256). Vilevile Ibn al-Mulaqqiyn ameafikiana naye katika “al-Khilaaswah al-Badr al-Muniyr”. Imaam Ahmad kabla ya watu hawa ameipa nguvu na akafanya hivo ni katika madhehebu yake. Abu Daawuud amesema:

“Nimemsikia Ahmad akiulizwa juu ya mwanaume ambaye amemwingilia mkewe ilihali yuko na hedhi ambapo akajibu: “Ni uzuri ulioje wa Hadiyth ya ´Abdul-Humayd juu ya jambo hio.” Nikasema: “Unamaanisha hivi ndivo unavoonelea?” Akasema: “Ndio, hiyo ndio kafara yake.” Nikasema: “Je, ni dinari moja au nusu ya dinari?” Akajibu: “Vile upendavyo.” al-Masaa-il (26)

Kundi la Muhaddithuun wengine katika Salaf wameonelea kuitendea kazi Hadiyth. as-Shawkaaniy ameyataja majina yao katika “an-Nayl” (01/244) na akaipa nguvu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 122
  • Imechapishwa: 12/03/2018