[4] Inajuzu kwa mwanamke kumtembelea mume wake wakati anapofanya I´tikaaf kama ambavyo inafaa kwake mwanamume kumuaga kwenye mlango wa msikiti. Swafiyyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya I´tikaaf [msikitini katika yale masiku kumi ya mwisho ya Ramadhaan] pindi siku moja nilipomwendea kumtembelea. [Wakeze walikuwa tayari huko lakini wakaenda baada ya muda] na tukazungumza [kwa muda]. Halafu nikasimama ili nende [ndipo akasema: “Usiwe na harak; wacha tufuatane.”] Ndipo akasimama ili kunifuata.” Makazi yake yalikuwa nyumbani kwa Usaamah bin Zayd. [Pindi tulipofika kwenye mlango wa msikiti karibu na mlango wa Umm Salamah] wakapita pambizoni wanaume wawili kutoka katika Answaar. Pindi walipomuona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wakaanza kuchapuka. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Tulieni! Huyu ni Swafiyyah bint Huyayy.” Ndipo wakasema: “Ametakasika Allaah! Ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Hakika shaytwaan anatembea kwa mwanaadamu kama inavyotembea damu. Hakika mimi nachelea shari – au kitu – isije kuingia nyoyoni mwenu.””[1]

Inajuzu kwake kufanya I´tikaaf na mume wake au peke yake. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Moja ya wakeze Mtume wa Allaah alifanya I´tikaaf pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati akitokwa na damu ya ugonjwa (na katika upokezi mwingine inasemekana kwamba alikuwa ni Umm Salamah). Alikuwa akiona majimaji mekundu na manjano na hivyo wakati mwingine tulikuwa tunaweza kuweka sahani chini yake na huku anaswali.”[2]

Amesema vilevile:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya I´tikaaf yale masiku kumi ya mwisho ya Ramadhaan mpaka pale Allaah (´Azza wa Jall) alipomfisha.”[3]

[5] Kitendo hichi kinabatilishwa na jimaa kujengea maneno Yake (Ta´ala):

 وَلَا تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ

“Na wala msichanganyike nao hali ya kuwa nyinyi ni wenye kukaa I’tikaaf  misikitini.”[4]

Ibn ´Abbaas amesema:

“Yule mwenye kufanya I´tikaaf akifanya jimaa, basi I´tikaaf yake inabatilika na anatakiwa kuanza mwanzo.”[5]

Hata hivyo halazimiki kutoa kafara kwa sababu haikuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake.

Kutakasika kutokamana na mapungufu na himdi zote ni Zako Allaah. Nashuudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Wewe. Ninakuomba msamaha na kutubia Kwako.

Mpaka hapa yanaisha marejeo na masahihisho mapya na zile faida mpya zilizoongezwa na mwandishi. Haya yalikuwa siku ya jumapili tarehe 26 Rajab mwaka 1406 na swalah na salaam zimwendee yule ambaye hakuwa mjuzi wa kuandika wala kusoma Muhammad, familia yake na Maswahabah wake.

[1] Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim na Abu Daawuud na nyongeza ya mwisho ni ya kwake.

[2] Ameipokea al-Bukhaariy. Imetajwa katika “Swahiyh Abiy Daawuud” (2138). Upokezi mwingine unatoka kwa Sa´iyd bin Mansuur kama ilivyotajwa katika “al-Fath” (04/281). Hata hivyo ad-Daarimiy amesema kuwa anaitwa Zaynab (1/22) – na Allaah ndiye anajua zaidi.

[3] Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim na wengineo. Takhriyj yake imeshatangulia kutajwa.

[4] 02:183-187

[5] Ameipokea Ibn Abiy Shaybah (03/92) na ´Abdur-Razzaaq (04/363) kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qiyaam Ramadhwaan, uk. 39-41
  • Imechapishwa: 07/05/2019