17. Huwezi kujua vitenguzi vya Uislamu mpaka kwa kusoma


Huwezi kujua vitenguzi hivi, utata na fikira zilizopinda isipokuwa kwa elimu yenye manufaa. Mjinga anaweza kutumbukia katika mambo haya na huku hajui. Bali yeye anawafuata tu watu kichwa mchunga na wale ambao anawadhania vizuri. Matokeo yake anafanya kama wanavofanya.

Kuhusu mwanachuoni wa kisawasawa inafaa elimu yake kwa idhini ya Allaah. Anajiepushe na mambo haya. Yule ambaye anamtambua Allaah zaidi ndiye ambaye anamcha Allaah zaidi. Mtu anatakiwa kujifunza elimu yenye manufaa na khaswa khaswa elimu ya ´Aqiydah. Anatakiwa kuijua ´Aqiydah sahihi ili aweze kushikamana nayo. Sambamba na hilo ajue vitenguzi vya ´Aqiydah na vitu vinavyoiharibu ´Aqiydah ili aweze kuviepuka. Hudhayfah bin al-Yamaan amesema:

“Watu walikuwa wakimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu mambo ya kheri na mimi nilikuwa nikimuuliza kuhusu shari ili isije kunikumba.”[1]

Huu ndio uelewa. Hakuitakasa nafsi yake. Amesema:

“…ili isije kunikumba.”

Sisi hii leo tuko katika fitina kubwa kukiwemo shubuha zenye kupotosha, walinganizi waovu na mambo mengine mengi ambayo yanatambulika. Kwa hivyo ni wajibu kwa mtu kutilia umuhimu jambo la dini yake na aikhofie.

[1] Ameipokea al-Bukhaariy (3606) na Muslim (1847) kupitia kwa Hudhayfah bin al-Yamaan (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 38
  • Imechapishwa: 26/06/2018