17. Hekima ya kuingiza kaburi la Mtume msikitini

Swali: Kama inavotambulika haijuzu kuwazika waliokufa misikitini na aidha haijuzu kuswali ndani ya msikiti ulio na kaburi. Ni ipi hekima ya kuingiza kaburi lake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na baadhi ya Maswahabah zake ndani ya msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?

Jibu: Hakika imethibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

”Allaah awalaani mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni mahali pa kuswalia.”[1]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Vilevile imethibiti kupitia kwa ´Aaishah na Umm Salamah kwamba walimtajia Mtume Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kanisa aliyoiona Habashah na namna ilivyokuwa mapicha. Akasema:

“Hao ndio wale ambao wanapofiwa na mtu mwema au mja mwema, basi hujenga juu ya kaburi lake msikiti na huchora ndani yake picha hiyo. Hao ndio viumbe waovu kabisa mbele ya Allaah.”[2]

Kuna maafikiano juu yake.

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Jundub bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kwamba amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Hakika Allaah amenifanya kuwa kipenzi Wake wa karibu kama alivyomfanya Ibraahiym kuwa kipenzi Wake wa karibu. Na lau ningemchukua yeyote katika Ummah wangu kuwa kipenzi wangu wa karibu, basi ningelimfanya Abu Bakr kuwa kipenzi  wangu wa karibu. Tanabahini! Hakika wale waliokuwa kabla yenu walikuwa wakiyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa mahali pa kuswalia. Tanabahini! Msiyafanye makaburi kuwa mahali pa kuswalia. Hakika mimi nawakatazeni na hilo.”[3]

Muslim amepokea tena kupitia kwa Hadiyth ya Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kwamba amekataza kulitia chokaa kaburi, kukaa juu yake na kujenga juu yake.”[4]

Hadiyth hizi Swahiyh na nyenginezo zilizo na maana yake zote zinafahamisha uharamu wa kuijenga misikiti juu ya makaburi na amemlaani mwenye kufanya hivo. Ni kama ambavo zinaharamisha kujenga juu ya makaburi, kujenga makuba juu yake na kuiweka chokaa. Kwa sababu mambo hayo ni miongoni mwa sababu za shirki na kuwaabudia wenye nayo badala ya Allaah, kama yalivyotokea hapo zamani na hivi sasa.

Kwa hiyo ni lazima kwa waislamu kutahadhari na yale aliyokataza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na asidanganyike na yale yanayofanywa na watu wengi. Haki ni kitu kilichompotea muumini. Pindi anapokipata basi hukichukua. Haki inatambulika kwa dalili kupitia katika Qur-aan na Sunnah; na si kwa maoni na matendo ya watu.

Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na marafiki zake wawili (Radhiya Allaahu ´anhumaa) hawakuzikwa ndani ya msikiti. Alizikwa nyumbani kwa ´Aaishah. Lakini wakati ulipopanuliwa msikiti katika zama za al-Waliyd bin ´Abdil-Malik ndipo kikaingizwa chumba ndani ya msikiti mwishoni mwa karne ya kwanza. Kitendo chake hichi hakizingatiwi kuwa na hukumu moja ya kuzika ndani ya msikiti. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na marafiki zake hawakuzikwa kwenye ile ardhi ya msikiti. Kilichofanyika ni kuingiza kile chumba walichokuwemo ndani ya msikiti kwa sababu ya kuupanua

msikiti. Kwa sababu hiyo haiwezi kuwa hoja kwa yeyote juu ya kufaa kujenga juu ya makaburi, kuijenga misikiti juu yake au kuzika ndani yake kutokana na zile Hadiyth Swahiyh tulizozitaja punde kidogo zinazokataza jambo hilo. Kitendo cha al-Waliyd ndani yake hakuna hoja katika yale yanayokwenda kinyume na Sunnah iliyothibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] al-Bukhaariy (436) na Muslim (529).

[2] al-Bukhaariy (427) na Muslim (528).

[3] Muslim (532).

[4] Muslim (970).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 74-76
  • Imechapishwa: 05/05/2022