17. Haniyfiyyah ndio dini ya Ibraahiym (صلى الله عليه وسلم)

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Tambua – Allaah akuongoze katika utiifu Wake – kwamba Haniyfiyyah ndio dini na njia ya Ibraahiym; nako ni kule kumuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia Yeye dini.

MAELEZO

 Tumeshatangulia kuzungumzia kuhusu ujuzi na hivyo hakuna haja ya kuyarudi tena hapa.

Uongofu – Kushikamana na njia ya haki.

Utiifu – Kuafikiana na malengo kwa kufanya yaliyoamrishwa na kuacha yaliyokatazwa.

Haniyfiyyah – Ni dini iliyojitenga mbali na shirki na iliyojengwa juu ya kumtakasia nia Allaah (´Azza wa Jall).

Mila – Ni njia yake ya kidini aliyopita juu yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Ibraahiym – Ni rafiki wa karibu wa Mwingi wa rehema. Allaah (´Azza wa Jalla) amesema:

وَاتَّخَذَ اللَّـهُ إِبْرَاهِيمَ خَلِيلًا

“Allaah amemfanya Ibraahiym kuwa ni kipenzi wa karibu.” (an-Nisaa´ 04 : 125)

Yeye ndiye baba wa Mitume na mfumo na mwenendo wake umetajwa mara nyingi ili kumfanya kiigizo chema cha kuigilizwa.

Nako ni kule kumuabudu Allaah pekee – Neno ´ibaadah kwa ufahamu wake wenye kuenea maana yake ni kumdhalilikia Allaah hali ya kumpenda na kumuadhimisha kwa kutekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake kwa mujibu wa Shari´ah Yake.

Kuhusu ufahamu maalum  na upambanuzi wa neno ´ibaadah, Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“´Ibaadah ni neno lililokusanya kila anachokipenda Allaah na kukiridhia, katika maneno na matendo, yaliyodhahiri na yaliyojificha. Kama mfano wa khofu, woga, kutegemea, kuswali, kufunga, zakaah na mengineyo katika Shari´ah za Kiislamu.”

Kwa kumtakasia Yeye dini – Ikhlaasw ni kule kusafisha. Maana yake ni kule mtu kwa ´ibaadah Yake anayofanya kukusudia uso wa Allaah na kufika katika Nyumba Yake ya neema kwa njia ambayo hamwabudu yeyote pamoja Naye; si Malaika aliyekaribu wala Mtume aliyetumilizwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

ثُمَّ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ أَنِ اتَّبِعْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۖ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

“Kisha Tukakufunulia Wahy kwamba fuata mila ya Ibraahim, iliyojiepusha na shirki na kuielekea Tawhiyd, na hakuwa miongoni mwa washirikina.” (an-Nahl 16 : 123)

وَمَن يَرْغَبُ عَن مِّلَّةِ إِبْرَاهِيمَ إِلَّا مَن سَفِهَ نَفْسَهُ ۚ وَلَقَدِ اصْطَفَيْنَاهُ فِي الدُّنْيَا ۖ وَإِنَّهُ فِي الْآخِرَةِ لَمِنَ الصَّالِحِينَ  إِذْ قَالَ لَهُ رَبُّهُ أَسْلِمْ ۖ قَالَ أَسْلَمْتُ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ وَوَصَّىٰ بِهَا إِبْرَاهِيمُ بَنِيهِ وَيَعْقُوبُ يَا بَنِيَّ إِنَّ اللَّـهَ اصْطَفَىٰ لَكُمُ الدِّينَ فَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ

“Na nani atakayejitenga na mila ya Ibraahiym isipokuwa anayeitia nafsi yake upumbavu? Na kwa hakika Tumemteua duniani naye Aakhirah ni miongoni mwa wema. Mola wake alipomwambia: “Jisalimishe.” Akasema: “Nimejisalimisha kwa Mola wa walimwengu.” Na Ibraahiym akawausia hayo wanawe na Ya’quub: “Enyi wanangu! Hakika Allaah amekuchagulieni nyinyi dini; hivyo basi msife isipokuwa nyinyi ni waislamu.” (al-Baqarah 02 : 130-132)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 36-38
  • Imechapishwa: 19/05/2020