168. Ni yepi yanayomlazimu mwanamke ambaye amefiwa na mume wake?

Swali 168: Dada anauliza ni yepi yanayomlazimu mwanamke ambaye amefiwa na mume wake[1]?

Jibu: Imepokelewa katika Hadiyth mambo ambayo anatakiwa kujiepusha nayo anayekaa eda. Kuna mambo matano yanayotakikana kwake:

1 – Kulazimiana na nyumba ambayo amekufa ndani yake mume wake ilihali anaishi ndani yake. Atatakiwa kubaki hapo mpaka pale itakapomalizika eda. Eda yake ni miezi minne na siku kumi. Isipokuwa akiwa ni mjamzito. Atatoka katika eda yake kwa kule kujifungua ujauzito wake. Allaah (Subhaanah) amesema:

وَأُولَاتُ الْأَحْمَالِ أَجَلُهُنَّ أَن يَضَعْنَ حَمْلَهُنَّ

“Na wenye mimba muda wao [wa eda] watakapozaa mimba zao.”[2]

Asitoke ndani yake isipokuwa kwa mahitaji au dharurah kama vile kwenda hospitali wakati anapoumwa, kununua anachohitaji sokoni kama mfano wa chakula na vyenginevyo akiwa hana awezaye kumsimamia mambo hayo. Vivyo hivyo kama nyumba itabomoka basi atatakiwa kutoka ndani yake na kwenda katika nyumba nyingine. Sababu nyingine kama hana ambaye anaweza kumliwaza na anachelea juu ya nafsi yake, basi katika hali hiyo hapana vibaya kwa yeye wakati wa haja.

2 – Haifai kwake kuvaa mavazi ya mapambo; si ya manjano, ya kijani wala nyingine. Avae mavazi yasiyokuwa ya mapambo. Ni mamoja ni meusi, ya kijani au mengine. Muhimu vazi lisiwe la mapambo. Hivi ndivo alivyoamrisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

3 – Ajiepushe na mapambo katika dhahabu, fedha, almasi, lulu na mfano wake. Ni mamoja iwe shanga, bangili, pete na mfano wake mpaka eda imalizike.

4 – Ajiepushe na manukato. Asijitie manukato si kwa uvumba wala manukato sampuli nyingine. Isipokuwa katika hali ya kutwahirika kutokamana na hedhi peke yake. Hapo hakuna neno kujitia manukato kidogo.

5 – Ajiepushe na wanja. Haifai kwake kujitia wanja wala kitu chenye maana ya wanja katika vinavyoupamba uso. Tunakusudia urembo maalum ambao pengine akawafitinisha watu kwao. Kuhusu kujipamba kwa kawaida kwa maji na sabuni hapana vibaya. Lakini wanja unaopamba macho mawili na vyenginevyo vinavyofanana na wanja katika vitu ambavyo vinafanywa na wanawake usoni. Haya asiyafanye.

Mambo haya matano anatakiwa kuyahifadhi yule ambaye amefiwa na mume wake.

Kuhusu yale yanayodhaniwa na baadhi ya wasiokuwa na elimu na na wakazua ya kwamba eti asimzungumzishe yeyote, eti asizungumze na simu, eri asioge wiki nzima isipokuwa mara moja, eti atembee miguu peku, eti asitoke kwenye nuru ya mwezi na mfano wa mambo ya ukhurafi kama haya hayana msingi wowote. Bali inafaa kwake kutembea nyumbani kwake akiwa miguu peku na akiwa na viatu, akidhi mahitaji yake nyumbani, apike chakula chake na chakula cha wageni wake, atembee chini ya kivuli cha mwezi kwenye paa na kwenye bustani ya nyumbani, aoge pale anapotaka, amzungumze amtakaye maneno yasiyokuwa na mashaka, apeane  mikono na wanawake na vivyo hivyo Mahaarim zake. Kuhusu wasiokuwa Mahaarim zake haifai.

Inafaa kuondoa mtandio juu ya kichwa chake akiwa mbele ya Mahram zake. Asitumie hina, zafarani wala manukato  katika nguo wala kahawa. Kwa sababu zafarani ni aina moja wapo ya manukato. Vilevile haijuzu kwake kuchumbiwa. Lakini hapana vibaya kufanyiwa ishara. Kuhusu kumuwekea wazi kwamba anataka kuchumbiwa haifai.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (22/188-190).

[2] 65:04

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz, uk. 124-126
  • Imechapishwa: 31/01/2022