167. Hukumu zinazohusiana na eda ya aliyefiwa na mumewe

Swali 167: Ni yepi yaliowekwa katika Shari´ah kwa mwanamke aliyekaa eda kwa sababu ya kufiwa[1]?

Jibu: Ni lazima kwake kukaa eda kwa kipindi cha miezi minne na siku kumi akiwa si mwenye ujauzito. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَالَّذِينَ يُتَوَفَّوْنَ مِنكُمْ وَيَذَرُونَ أَزْوَاجًا يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا

“Na wale wanaofishwa miongoni mwenu na wakaacha wake, hao wake wangojee peke yao [eda ya] miezi minne na siku kumi.”[2]

Isipokuwa akiwa mjamzito. Katika hali hiyo eda yake itamalizika kwa kujifungua. Allaah (Subhaanah) amesema:’

وَأُولَاتُ الْأَحْمَالِ أَجَلُهُنَّ أَن يَضَعْنَ حَمْلَهُنَّ

“Na wenye mimba muda wao [wa eda] watakapozaa mimba zao.”[3]

Ni lazima kwake kujiepusha na mavazi ya mapambo, kutia wanja na manukato. Isipokuwa akitwahirika kutoka katika hedhi yake ni sawa akatia manukato kidogo. Vilevile analazimika kujiepusha na mapambo ya dhahabu na fedha na mengineyo. Analazimika vilevile kujiepusha na hina mikononi na kichwani mwake. Achane nywele zake kwa mkunazi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemkataza mwanamke mwenye kukaa eda tuliyoyataja.

Hapana vibaya kutumia shampoo, sabuni na Ashnaan[4]. Kwa sababu hayo hayaingii katika makatazo.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (22/187).

[2] 02:234

[3] 65:04

[4] Tazama https://en.wikipedia.org/wiki/Saltwort

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz, uk. 123
  • Imechapishwa: 31/01/2022