166. Haikuthibiti kumfanyia maiti ´Aqiyqah

Swali 166: Ni ipi hukumu ya Allaah na Mtume Wake juu ya watu ambao anapokufa mmoja katika wao basi jamaa zake wanamchinjia kondoo ambaye wanamwita “´Aqiyqah” na wala hawavunji mfupa wake wowote. Baada ya hapo wanazika mifupa na kinyesi chake na wanadai eti kufanya hivo ni vizuri na inapasa watu wayafanyie kazi[1]?

Jibu: Kitendo hichi ni Bid´ah na hakina msingi wowote katika Shari´ah ya Kiislamu. Kwa hiyo ni lazima kukiacha na kutubu kwa Allaah kutokamana nacho kama zilivyo Bid´ah na maasi mengine yote. Hakika kutubu kwa Allaah (Subhaanah) kunatulazimu sisi sote. Amesema (´Azza wa Jall):

وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

“Tubuni kwa Allaah nyote, enyi waumini, mpate kufaulu.”[2]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّـهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا

“Enyi walioamini! Tubieni kwa Allaah tawbah ya kwelikweli.”[3]

´Aqiyqah iliowekwa katika Shari´ah iliopokelewa na Sunnah Swahiyh kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni ile anayochinjiwa mtoto katika siku ya saba. Mtoto wa kiume atachinjiwa kondoo/mbuzi wawili na kondoo/mbuzi mmoja kwa mtoto wa kike.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimfanyia ´Aqiyqah al-Hasan na al-Husayn (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Mwenye nayo ana khiyari; akitaka atawagawia nyama ndugu jamaa, marafiki na mafukara na akitaka ataipika na kuwaalika awatakao katika ndugu jamaa, majirani na mafukara. Hii ndio ´Aqiyqah iliowekwa katika Shari´ah. Ni Sunnah iliokokotezwa. Mwenye kuiacha hakuna dhambi juu yake.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (13/423-424).

[2] 24:31

[3] 66:08

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz, uk. 121-122
  • Imechapishwa: 31/01/2022