Swali 163: Nilimwambia kaka yangu nitapokufa basi asinililie na wala asitangaze kwenye maikrofonia. Mimi nachelea kuwa atafanya hivo. Ni yepi maelekezo yako[1]?

Jibu: Ni lazima kwa waislamu katika katika mambo haya wawe na subira na watarajie malipo kutoka kwa Allaah na wasiomboleze, wasipasue nguo, wasijipige mashavu na mfano wa hayo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Si katika mimi yule atayejipiga mashavu, akapasua nguo na akaita wito wa kipindi cha kikafiri.”[2]

Amesema vilevile (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth Swahiyh:

“Mambo mane katika Ummah wangu ni miongoni mwa mambo ya kipindi cha kikafiri na hawatoyaacha; kujifakhari kwa ukoo, kutukaniana nasaba, kuinasibisha mvua kwa nyota na kuomboleza.”

Vilevile amesema:

“Mwanamke mwenye kuomboleza ikiwa hakutubia kabla ya kufa kwake, basi atafufuliwa siku ya Qiyaamah na huku akiwa amevishwa nguo ya shaba iliyoyeyuka na kanzu ya ukoma.”[3]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Kuomboleza ni kunyanyua sauti wakati wa kumlilia maiti. Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mimi najitenga mbali na mwanamke anayenyanyua sauti yake, anayenyoa nywele zake na anayepasua nguo zake wakati wa msiba.”[4]

Yote haya ni katika ni katika kukata tamaa. Haijuzu kwa mwanamke wala mwanamme kufanya chochote katika hayo. Ni lazima kwa familia yako kukubali wasia huu na watahadhari kutokamana na kukufanyia maombolezo. Kwa sababu maombolezo yanawadhuru wao na yanamdhuru vilevile maiti. Imepokelewa katika Hadiyth Swahiyh:

“Maiti anaadhibiwa ndani ya kaburi lake kwa kufanyiwa maombolezi.”[5]

Kwa hiyo haijuzu kwao kumfanyia mambolezo maiti.

Kuhusu kulia kwa maana ya kutiririkwa na machozi na moyo kuhuzunika hapana vibaya. Kulichokatazwa ni kunyanyua sauti kwa mayowe. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipofariki mwanawe Ibraahiym:

“Hakika macho hutokwa na machozi na moyo huingiwa na huzuni na wala hatusemi isipokuwa yale yenye kumridhisha Mola wetu. Hakika sisi ni wenye kuhuzunika kwa kutengana na wewe Ibraahiym.”[6]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah haadhibu kwa machozi ya macho wala kwa huzuni wa moyo. Lakini anaadhibu au kurehemu kwa hichi – na akaashiria ulimi.”[7]

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (13/413).

[2] al-Bukhaariy /(1212) na tamko ni lake, na Muslim (148).

[3] Muslim (934).

[4] al-Bukhaariy (03/165 – Fath) na Muslim (104).

[5] al-Bukhaariy (1210) na Muslim (1537).

[6] al-Bukhaariy (1303) na tamko ni lake, na Muslim (2315).

[7] al-Bukhaariy (1221) na Muslim (1532).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz, uk. 118-120
  • Imechapishwa: 02/02/2022