22- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameharamisha mambo yaliyokuweko na bado mpaka sasa baadhi ya watu wanayafanya wanapofiwa na maiti. Kwa hivyo ni lazima kuyatambua ili watu wajiepushe nayo. Ni lazima kuyabainisha:

1- Kuomboleza[1]. Kuhusu hilo kumepokelewa Hadiyth nyingi:

“Katika Ummah wangu kuna mambo mane ya kipindi cha kishirikina ambayo hayatoachwa; kujifakharisha kwa kabila, kutukaniana nasabu, kuinasibisha mvua na nyota na kuomboleza.”

Vilevile amesema:

“Mwanamke mwenye kuomboleza na asitubie kabla ya kufa, basi atafufuliwa siku ya Qiyaamah akiwa amevaa mavazi ya lami na kanzu ya ukurutu.”

Ameipokea Muslim (01/45), al-Bayhaqiy (04/63) kupitia kwa Abu Maalik al-Ash´ariy.

A- “Mambo mawili kwa watu ni ukafiri; kutukaniana nasabu na kuomboleza juu ya maiti.”

Ameipokea Muslim (01/58), al-Bayhaqiy (04/63) na wengineo kupitia kwa Abu Hurayrah.

B- “Wakati alipokufa Ibraahiym, mwana wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Usaamah bin Zayd alipiga makelele. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Huyu si katika mimi na mwenye kupiga makele hana haki. Moyo huhuzunika, macho yakatiririkwa na machozi na hakasirishwi Mola.”

Ameipokea Ibn Hibbaan (743) na al-Haakim (01/382) kupitia kwa Abu Hurayrah kwa mlolongo wa wapokezi mzuri.

C- Umm ´Atwiyyah amesimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alichukua kutoka kwetu, sambamba na kiapo cha usikivu, tusiomboleze. Hakuna mwanamke yeyote katika sisi aliyetimiza [akimaanisha katika wale waliokula viapo] isipokuwa wanawake watano; Umm Sulaym, Umm-ul-´Alaa´, msichana wa Abu Swabrah ambaye ni mke wa Mu´aadh, au ni msichana wa Abu Swabrah na mke wa Mu´aadh.”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/137), Muslim (03/46) na tamko ni lake, al-Bayhaqiy (04/62) na wengineo.

D- Anas bin Maalik ameeleza:

“Wakati ´Umar bin al-Khattwaab alipodungwa Hafswah akamlilia kwa sauti. Akasema: “Ee Hafswah! Hukumsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema: “Mwenye kulia kwa kupiga kunyanyua sauti ataadhibiwa?” Pia Swuhayb akamlilia kwa sauti. [Akisema: “Ee ndugu yangu! Ee rafiki yangu!] ´Umar akasema: “Ee Swuhayb! Hivi hukujua kwamba mwenye kuliliwa kwa sauti huadhibiwa?” [Katika upokezi mwingine]: “Hakika maiti ataadhibiwa kwa baadhi ya vilio vya jamaa zake juu yake. Katika upokezi mwingine imekuja: “[Ndani ya kaburi lake] kwa kule kuliliwa juu yake.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim – na mtiririko ni wake –, al-Bayhaqiy (04/72-73), Ahmad (nambari. 288, 290, 315, 334, 254, 386) kupitia kwa ´Umar kwa kirefu na kwa kifupi. Pia Ibn Hibbaan ameipokea katika “as-Swahiyh” yake (741) kisa cha Hafswah peke yake.

E- “Hakika maiti ataadhibiwa kwa vilio vya jamaa zake juu yake.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Maiti ataadhibiwa ndani ya kaburi lake kwa kwa kule kuliliwa juu yake.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim na Ahmad kupitia kwa Ibn ´Umar. Upokezi mwingine ni wa Muslim na Ahmad. Ibn Hibbaan amepokea katika “as-Swahiyh” yake (742) kupitia kwa ´Imraan bin Huswayn mfano wa upokezi wa kwanza.

F- “Mwenye kuliliwa kwa sauti ataadhibiwa kwa yale aliyoliliwa kwa sauti (siku ya Qiyaamah).”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/126), Muslim (03/45), al-Bayhaqiy (04/72) na Ahmad (04/235, 252, 255).

Katika Hadiyth hizi kuna ubainifu kwamba kilio kilichotajwa katika Hadiyth ilio kabla yazo makusudio sio vilio moja kwa moja. Bali hivyo ni vilio maalum, ambavyo ni kwa kuomboleza. Hadiyth ya ´Umar iliotangulia katika upokezi wa pili imeashiria jambo hilo. Hadiyth hiyo ni ile isemayo:

“Hakika maiti ataadhibiwa kwa baadhi ya vilio vya jamaa zake juu yake.”

Jengine ni kwamba udhahiri wa Hadiyth hii na zile mbili zilizo kabla yake ni mushkili, kwa sababu zinakinzana na baadhi ya misingi ya ki-Shari´ah na kanuni zake zenye kuthibitishwa katika mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ

“Wala habebi mbebaji mzigo dhambi za mwengine.”[2]

Wanachuoni wametofautiana katika kuyajibu hayo katika maoni nane. Maoni yaliyo karibu zaidi na usawa ni mawili:

Ya kwanza: Maoni waliyoonelea wanachuoni wengi. Wamesema kwamba Hadiyth ni yenye kufasiriwa juu ya kwamba ni kwa yule aliyeacha anausia kuliliwa au hakuacha anausia kutoliliwa pamoja na kwamba alijua desturi zao watu hufanya hivo. Kwa ajili hiyo ´Abdullaah bin al-Mubaarak amesema:

“Ikiwa alikuwa anawakataza kipindi cha uhai wake ambapo wakafanya kitu katika hayo baada ya kufa kwake, hatopatwa na chochote.”[3]

Wanachuoni hao wanaona kuwa adhabu ni kwa maana ya kuteswa.

Ya pili: Maana ya neno “ataadhibiwa” ni kwamba atapatwa na maumivu kwa kule kusikia vilio vya jamaa zake na huhuzunika kwa ajili yao. Hayo hutokea ndani ya kaburi na sio siku ya Qiyaamah. Muhammad bin Jariyr at-Twabariy pia na wengineo wameonelea hivo. Ameyasunuru maoni hayo Ibn Taymiyyah, Ibn-ul-Qayyim na wengineo na wakasema:

“Haina maana kwamba Allaah atamuadhibu kwa kumtsea kwa kule jamaa zake waliohai kumlilia. Adhabi ni maana ilioenea zaidi kuliko kuteswa, kama ilivyokuja katika maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Safari ni kipande cha adhabu.”[4]

Hii sio adhabu kwa dhambi aliyoifanya. Bali huku ni kuteseka na kuhisi maumivu.”

Hili linaweza kutiliwa nguvu na maneno yake katika Hadiyth namba 05 na 06: “Ndani ya kaburi lake”. Nilikuwa ni mwenye kumili juu ya madhehebu haya kwa muda muda fulani katika zama. Kisha ikanidhihirikia kuwa ni dhaifu kwa sababu ya inaenda kinyume na Hadiyth ya saba ambayo imefungamanisha adhabu kwamba ni “Siku ya Qiyaamah”. Miongoni mwa mambo yaliyo wazi ni kwamba hili haliwezi kufasiriwa kwa yaliyotajwa. Kwa ajili hiyo tunaona kuwa maoni yenye nguvu ni yale ya wanachuoni wengi. Hakuna kupingana kati ya kifungamanishi hiki na kifungamanishi kingine ambapo amesema “Ndani ya kaburi”. Bali moja linaegemezwa kwenye lingine na natija inakuja kwamba ataadhibiwa ndani ya kaburi lake na siku ya Qiyaamah, jambo ambalo liko wazi – Allaah akitaka.

G- an-Nu´maan bin  Bashiyr ameeleza:

“´Abdullaah bin Rawaahah (Radhiya Allaahu ´anh) alizimia. Dada yake ´Amrah akawa analia: “Ee nguzo yangu! Ee kadhaa! Ee kadhaa!” na mengi ya hayo.” Alipozinduka akasema: “Hukusema kitu isipokuwa nilikuwa nikiambiwa: “Ni kweli wewe uko hivyo?” Alipokufa hakumlilia tena.”

Ameipokea al-Bukhaariy na al-Bayhaqiy (04/64).

Katika maudhui haya zipo Hadiyth zengine ambazo tutazitaja katika sura zengine – Allaah (Ta´ala) akitaka.

Katika maudhui haya zipo Hadiyth zengine ambazo tutazitaja katika sura zengine – Allaah (Ta´ala) akitaka.

[1] Ni jambo lenye kuzidi juu ya kulia. Ibn ´Arabiy amesema:

“Na´y (kuomboleza) ni yale yaliyokuwa yakifanywa katika kipindi cha kikafiri. Wanawake walikuwa wakikaa hali ya kuwa wametazamana wanalia, wakijimwagia mchanga juu ya vichwa vyao, wakijipiga vichwa vyao.” Haya yamenakiliwa na al-Ubbiy katika “Sharh” yake ya “Swahiyh-ul-Muslim”.

[2] 06:164

[3] ´Umdat-ul-Qaariy (04/79).

[4] Tazama maneno ya Ibn Taymiyyah katika ”Majmuu´ah ar-Rasaa-iyl al-Muniyriyyah (02/209) na Ibn-ul-Qayyim katika ”Tahdhiyb-us-Sunan” (04/290-293).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 39-42
  • Imechapishwa: 31/12/2019