16. Unafiki ni kitu gani na umegawanyika sehemu ngapi na zipi sifa zake?

´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali: Unafiki ni kitu gani na umegawanyika sehemu ngapi na zipi sifa zake?

Jibu: Unafiki maana yake ni kuficha kheri na kuficha shari. Umegawanyika aina mbili:

1 – Unafiki mkubwa wenye kuhusiana na imani. Aliye na unafiki aina hii atadumishwa Motoni milele. Mfano wake ni kama yale aliyoelezea Allaah kuhusu wanafiki pale aliposema:

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ وَبِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَمَا هُم بِمُؤْمِنِينَ

“Na miongoni mwa watu wako wasemao: ”Tumemuamini Allaah na Siku ya Mwisho”, hali ya kuwa si wenye kuamini.” (02:08)

Hawa wanaficha ukafiri na wanaonesha imani.

2 – Unafiki mdogo wenye kuhusiana na matendo. Mfano wake ni kama yale aliyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Alama za mnafiki ni tatu; anapozungumza husema uongo, anapoahidi hatimizi na anapoaminiwa anasaliti.”[1]

Kufuru na unafiki mkubwa haunufaishi imani na matendo. Kuhusu kufuru na unafiki mdogo, unaweza kukusanyika sehemu moja na imani. Katika hali hii mja anakuwa na kheri na shari na anastahiki thawabu na adhabu vyote viwili.

MAELEZO

Unafiki ni neno limechukuliwa kutoka katika النفق, maana yake ni kuchimba ardhini. Utambulisho wake Kishari´ah ni kudhihirisha Uislamu na kuficha ukafiri. Kwa ujumla ni kudhihirisha kheri na kuficha shari.

Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofika Madiynah alikuwa anayetaka anaingia katika Uislamu na kumfuata na yule mwenye kutaka anabaki katika dini yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwalingania watu katika Uislamu; wako ambao walikuwa wakiingia katika Uislamu kwa kutaka kwao wenyewe na wengine wakibaki katika dini zao. Baadaye ilipotokea vita vya Badr na waislamu wakawapa nguvu basi hapo ndipo wanafiki waliambiana waonyeshe Uislamu na wafiche ukafiri. Ndipo wakaanza kuonyesha Uislamu chini ya uongozi wa ´Abdullaah bin Ubayy na wakati huohuo wakawa ni wenye kuficha ukafiri na kumkadhibisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Uislamu. Wanafiki hawa walikuwa ni wenye kujificha katika jamii ya Kiislamu. Pindi Allaah (´Azza wa Jall) alipoteremsha Suurah “at-Tawbah” na akaeleza:

وَمِنْهُم مَّن يَقُولُ ائْذَن لِّي وَلَا تَفْتِنِّي ۚ أَلَا فِي الْفِتْنَةِ سَقَطُوا ۗ وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمُحِيطَةٌ بِالْكَافِرِينَ

“Miongoni mwao yuko anayesema: “Niruhusu na wala usinifitini” Zinduka! Wamekwishaanguka katika fitina na hakika Jahannam imewazunguka makafiri.”[2]

وَمِنْهُم مَّن يَلْمِزُكَ فِي الصَّدَقَاتِ فَإِنْ أُعْطُوا مِنْهَا رَضُوا وَإِن لَّمْ يُعْطَوْا مِنْهَا إِذَا هُمْ يَسْخَطُونَ

“Miongoni mwao wako wanaokufedhehesha kwa kushutumu katika swadaqah. Wakipewa humo wanaridhika na wasipopewa humo, basi tahamaki wao hukasirika.”[3]

Zipo Aayah nyingi ambazo Allaah amefichua nyingi katika sifa zao. Sifa zao zilikuwa zenye kuonekana muda baada ya muda. Mfano wa hayo ni yale aliyosema ´Abdullaah bin Ubayy katika tukio la Banuul-Mustwalaq:

“Msaidieni ndugu yenu! Msimamo wetu kwa Muhammad ni kama ambaye alisema: “Mpe mbwa wako mafuta baadaye aje akule.”

Vilevile amesema:

لَئِن رَّجَعْنَا إِلَى الْمَدِينَةِ لَيُخْرِجَنَّ الْأَعَزُّ مِنْهَا الْأَذَلَّ

“Wanasema: “Tutakaporudi Madiynah, basi mwenye hadhi zaidi atamfukuza humo aliye mtevu!”[4]

Zayd bin Arqam (Radhiya Allaahu ´anh) akamsikia na kipindi hicho alikuwa ni kijana mdogo na akaenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumweleza aliyosema. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamtuma mjumbe kwake amuulize kama kweli amesema maneno hayo, ambapo akapinga na akaapa kwa jina la Allaah kwamba hakusema maneno hayo. Ndipo Answaar wakamkemea Zayd bin Arqam na baada ya hapo Allaah akateremsha Suurah “al-Munaafiquun:

إِذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ

”Watakapokujia wanafiki wakisema: “Tunashuhudia kwamba wewe bila shaka ni Mtume wa Allaah.” – na Allaah anajua vyema kuwa hakika wewe ni Mtume Wake na Allaah anashuhudia kuwa hakika wanafiki bila shaka ni waongo.”[5]

Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alishika sikio la Zayd bin Arqam na akasema:

“Huyu ndiye ambaye usikivu wake umethibitishwa na Allaah.”[6]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Allaah amekusadikisha, ee Zayd.”[7]

al-Hasan amesimulia pasi na Swahabah katika cheni ya wapokezi kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alishika sikio la ´Umayr bin Sa´d na akasema:

“Sikio lako lilipatia, ee ´Umayr, na Mola wako amekusadikisha.”[8]

Unafiki unaohusiana na imani ni mtu kusema kuwa ni muislamu, akashuhudia shahaadah, akaswali pamoja na watu wengine, wakati anapokuwa mwenyewe basi anaacha kuswali. Allaah amewasifia wanafiki kwa kusema:

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَىٰ يُرَاءُونَ النَّاسَ وَلَا يَذْكُرُونَ اللَّـهَ إِلَّا قَلِيلًا

“Hakika wanafiki wanamhadaa Allaah na hali Yeye ndiye Mwenye kuwahadaa na wanaposimama kuswali basi husimama kwa uvivu, wakijionyesha kwa watu na wala hawamtaji Allaah isipokuwa kidogo tu.”[9]

Watu kama hawa ni wenye kudumishwa Motoni milele; bali watakuwa kwenye tabaka la chini kabisa Motoni, kama alivoeleza Allaah[10].

Kuhusu unafiki mdogo ambao unahusiana na matendo ni kule kuonyesha kitu kimoja na kuficha kinyume chake. Mwongo anadai kuwa ni mkweli, ilihali ni mwongo kwa ndani. Mtu mwenye kuahidi anajidhihirisha kuwa ni mkweli katika ahadi yake, ilihali kwa ndani  ni kinyume na hivo. Pindi anapofanyiwa uaminifu, basi hufanya khiyana. Anawadhihirishia watu kuwa ni mwaminifu, ilihali ukweli wa mambo ni mkhaini. Kwa ajili hii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Alama za mnafiki ni tatu; anapozungumza husema uongo, anapoahidi hatimizi na anapoaminiwa anasaliti.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… anapoingia kwenye mkataba, basi husaliti… “

 Katika upokezi mwingine imekuja:

“… anapogombana, basi hufanya uasi… “[11]

Sifa hizi hazimtoi mtu nje ya Uislamu. Lakini mwenye kufanya hivo anabaki kuwa ni muislamu na mnafiki mwenye unafiki wa kimatendo. Mtu huyu ni kama watenda madhambi makubwa wengine wote ambapo anakuwa chini ya matakwa ya Allaah ima kumuadhibu au kumsamehe. Unafiki aina hii ni unafiki mdogo au pia unaweza kusema kuwa ni unafiki wa kimatendo. Waislamu wengi wanasifika na sifa hizi zilizotajwa ambazo ni mbaya. Hivyo mmoja katika wao anakuwa na sababu zote mbili zinazopelekea katika kupata thawabu na sababu zinazopelekea kupata adhabu. Ni kama tulivosema kwamba ni kama watenda madhambi makubwa wengine wote ambapo anakuwa chini ya matakwa ya Allaah ima kumuadhibu au kumsamehe.

[1] al-Bukhaariy (33) na Muslim (59).

[2] 9:49

[3] 09:58

[4] Jaami´-ul-Bayaan (14/364).

[5] 63:01-02

[6] Jaami´-ul-Bayaan (23/406-407).

[7] al-Bukhaariy (4900).

[8] ´Abdur-Razzaaq (10/45-46).

[9] 04:142

[10] Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ فِي الدَّرْكِ الْأَسْفَلِ مِنَ النَّارِ وَلَن تَجِدَ لَهُمْ نَصِيرًا

“Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka la chini kabisa katika Moto na wala hutompata kwa ajili yao mwenye kunusuru.” (04:145)

[11] al-Bukhaariy (34) na Muslim (58).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 90-93
  • Imechapishwa: 21/10/2021