16. Uharamu wa kumwingilia mwanamke mwenye hedhi


14- Uharamu wa kumwingilia mwenye hedhi

Ni haramu kwake mwanaume kumwingilia ndani ya hedhi[1] kutokana na maneno Yake (Ta´ala):

 وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ ۖ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ

“Wanakuuliza kuhusu hedhi. Sema: “Hiyo ni dhara, hivyo basi waepukeni wanawake katika hedhi. Wala msiwakaribie kujimai nao mpaka watwaharike.”[2]

Kumepokelewa Hadiyth kadhaa juu ya hilo:

1- Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kumwingilia mwenye hedhi, mwanamke kwenye tupu yake au kuhani na akamsadikisha kwa yale aliyoyasema basi amekufuru yale yaliyoteremshwa kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

2- Anas bin Maalik amesimulia:

“Pindi mwanamke mmoja wa mayahudi alipokuwa akiingia katika hedhi, basi wanamtoa nje ya nyumba na hawali naye, hawanywi naye na wala hawachanganyiki naye nyumbani. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akauliza juu ya hili ndipo Allaah (Ta´ala) akateremsha:

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ

“Wanakuuliza kuhusu hedhi… “

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Kaeni nao majumbani na fanyeni kila kitu isipokuwa tendo la ndoa.” Mayahudi wakasema: “Mtu huyu hakuna kitu tunachokifanya isipokuwa anataka ahakikishe ameenda kinyume na sisi. Usayd bin Khudhwayr na ´Abbaad bin Bishr wakaja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Hakika mayahudi wanasema kadhaa na kadhaa. Kwa nini tusifanye jimaa wakati wa hedhi [ili kwenda kinyume nao]? Tahamaki ndipo uso wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ukabadilika mpaka tukafikiri kuwa ametukasirikia. Wakatoka na wakakutana na zawadi ya maziwa alioletewa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akamtuma mtu awanywesheleze na hapo ndipo wakatambua kwamba hakuwakasirikia.”[3]

[1] ash-Shawkaaniy amesema:

“Hakuna tofauti kati ya wanachuoni juu ya uharamu wa kufanya jimaa na mwanamke mwenye hedhi. Ni jambo linalojulikana fika katika dini.” (Fath-ul-Qadiyr)

[2] 02:222

[3] Ameipokea Muslim, Abu ´Awaanah katika “as-Swahiyh” zao, Abu Daawuud kwa nambari. 250 katika “as-Swahiyh” yake na haya ni matamshi yake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 120-122
  • Imechapishwa: 12/03/2018