16. Ubishi katika kidini


Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Lililo juu yake ni kuziamini na asirudishe herufi hata moja kwenye Hadiyth hizo au nyenginezo zilizopokelewa kutoka kwa wapokezi waaminifu. Asivutane wala kubishana na yeyote. Wala asijifunze mijadala. Mizozano juu ya Qadar, Kuonekana, Qur-aan na mambo mengine ya I´tiqaad ni jambo limechukizwa na limekatazwa. Mwenye kufanya hivo sio katika Ahl-us-Sunnah – japokuwa atazungumza kwa ´Aqiydah – mpaka pale atapoacha mijadala na kujisalimisha na kuamini mapokezi.”

MAELEZO

Bila shaka katika mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na ´Aqiydah nzuri ni kwamba imekatazwa mijadala isiyokuwa na faida yoyote ambayo inapelekea katika shari na mpasuko. Makatazo yanahusiana na dini ya Allaah kwa jumla na khaswa katika majina na sifa za Allaah, Qadar, kuonekana kwa Allaah siku ya Qiyaamah na mengineyo. Hakuna nafasi ya kuyajadili mambo haya. Ni wajibu kwa waislamu kujisalimisha na kusadikisha maandiko na misingi mitukufu.

Pamoja na kwamba kunavuliwa mijadala yenye faida, bi maana inayobainisha haki na kuiweka wazi na kuraddi batili na kila chenye kuhusiana nayo, kuibainisha Sunnah na kila chenye kuhusiana nayo na kuiraddi Bid´ah na kila chenye kuhusiana nayo. Mijadala kama hii ni yenye kusifiwa na anapewa thawabu yule mwenye nayo. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

وَلَا تُجَادِلُوا أَهْلَ الْكِتَابِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“Wala msibishane na Ahl-ul-Kitaab isipokuwa kwa yale ambayo ni mazuri zaidi.”[1]

Ikiwa mjadala ni kwa njia ilio nzuri kwa lengo la kubainisha haki na Sunnah na kuraddi batili na Bid´ah, basi ni kulingania kwa Allaah (´Azza wa Jall) na kuifikisha elimu kwa wale wenye kuihitajia. Haki ikibainishwa kwa dalili na yule mwenye kufanya mjadala akaendelea kung´ang´ania juu ya ubishi wake na akasababisha mzozo, basi anatakiwa kuachwa. Sunniy asiendelee kujadiliana na mtu kama huyu. Ahl-ul-Bid´ah hueneza shubuha zao na hivyo kuna khatari wale wasikilizaji wakaja kuathirika kwa shubuha zao na zikakita mioyoni mwao. Matokeo yake wakaanza kumili kwa Ahl-ul-Bid´ah au kudangana juu ya jambo la kidini ambalo haijuzu kulitilia shaka au kuwa na mashaka nalo.

[1] 29:46

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 68-69
  • Imechapishwa: 08/10/2019