16. Sura ya tano: Ubainifu wa kwamba Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah inapelekea Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah

Maana ya hayo ni kwamba ambaye ataikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah ambapo akakubali kwamba hakuna muumbaji, mruzukaji na mwendeshaji ulimwengu isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall) basi itamlazimu akubali pia kwamba hakuna anayestahiki ´ibaadah kwa aina zake zote isipokuwa Allaah (Subhaanah). Hii ndio Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Uluuhiyyah ndio ´ibaadah. Mungu (al-Iaah) maana yake ni mwabudiwa. Haombwi mwengine isipokuwa Allaah. Hatakwi msaada mwengine asiyekuwa Allaah. Hategemewi mwengine asiyekuwa Allaah. Hakuchinjwi vichinjwa kwa lengo la kujikurubisha, hakuwekwi nadhiri wala hakufanywi aina yoyote ya ´ibaadah kwa ajili ya mwengine asiyekuwa Yeye. Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah ni dalili inayoonyesha ulazima wa Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Kwa ajili hii mara nyingi Allaah (Subhaanah) hutumia hoja dhidi ya wale wanaopinga Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah kwa yale wanayokubali kutoka katika Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Kwa mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu ambaye amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kucha. Ambaye amewafanyieni ardhi kuwa ni tandiko na mbingu kuwa ni paa na akateremsha kutoka mbinguni maji akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki zenu. Hivyo basi, msimfanyie Allaah washirika hali ya kuwa nyinyi mnajua [kwamba hana washirika].”[1]

Akawaamrisha Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Ametumia hoja dhidi yao kwa Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah ambayo ndio kuumbwa kwa watu kuanzia wa mwanzo mpaka wa mwisho, kuumbwa kwa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake, kudhalilisha pepo, kuteremsha mvua, kuotesha mazao na kutoa matunda ambayo ni riziki za waja. Kwa hivyo haiwastahikii wao kumshirikisha Yeye pamoja na wengine katika wale ambao wanajua kuwa hawakufanya chochote katika hayo wala mengineyo. Njia ya kimaumbile katika kuthibitisha Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah ni kuitumia kama mwongozo kwa Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Hakika mtu siku zote hufungamana na chanzo cha umbile lake na asili ya manufaa na madhara yake, kisha baada ya hapo anahama kwenda katika njia zinazomkurubisha kwavyo, zinazomridhisha na zinazokomaza mafungamano kati yake yeye na vitu hivyo. Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah ni mlango wa Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Kwa sababu hiyo ndio maana Allaah akawahoji washirikina kwa njia hiyo na akamwamrisha Mtume Wake kuwahoji kwayo. Amesema (Ta´ala):

قُل لِّمَنِ الْأَرْضُ وَمَن فِيهَا إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ السَّبْعِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ قُلْ مَن بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ يُجِيرُ وَلَا يُجَارُ عَلَيْهِ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ فَأَنَّىٰ تُسْحَرُونَ

“Sema: “Ni ya nani ardhi na wale waliokuwemo ndani yake mkiwa mnajua?” Watasema: “Ni ya Allaah pekee.” Sema: “Je, basi kwa nini hamkumbuki?” Sema: “Ni nani Mola wa mbingu saba na Mola wa ‘Arshi tukufu?” Watesema: “Ni ya Allaah pekee.” Sema: “Je, basi kwa nini hamchi?” Sema: ”Nani katika mikono Yake uko ufalme wa kila kitu Naye ndiye Alindae na wala hakilindwi chochote kinyume Naye ikiwa mnajua?” Watasema: ”Ni Allaah pekee.” Sema: “Basi vipi mnazugwa?”[2]

ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ فَاعْبُدُوهُ

”Huyo kwenu ndiye Allaah, Mola wenu, hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye Muumbaji wa kila kitu, basi mwabuduni Yeye pekee.”[3]

Ametumia dalili ya kupwekeka Kwake kwa uola juu ya kustahiki Kwake ´ibaadah.

Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah ndio ambayo wameumbwa viumbe kwa ajili yake. Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”[4]

Maana ya ´waniabudu` ni kwamba wanipwekeshe Mimi kwa ´ibaadah. Mja hawi ni mwenye kumwabudu Allaah pekee kwa kule kukiri kwake tu Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Ni lazima aikubali na kuitendea kazi Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Vinginevyo washirikina walikuwa wakiikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Hata hivo aikuwaingiza ndani ya Uislamu. Mtume wa Allaah (Swalla Allaau ´alayhi wa sallam)  aliwapiga vita licha ya kuwa wanakubali kwamba Allaah ndiye muumbaji, mruzukaji, muhuishaji na mfishaji. Amesema (Ta´ala):

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَهُمْ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ

“Ukiwauliza: “Ni nani kawaumba?” Bila shaka watasema: “Allaah.”[5]

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ خَلَقَهُنَّ الْعَزِيزُ الْعَلِيمُ

”Ukiwauliza:  ”Ni nani yule aliyeumba mbingu na ardhi?” Hakika watasema: ”Ameziumba Mwenye nguvu kabisa asiyeshindika, Mjuzi wa yote.”[6]

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ

”Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini au nani anayemiliki kusikia na kuona na nani anayemtoa aliye hai kutoka mfu na anayemtoa mfu kutoka aliye hai na nani anayeendesha mambo?”  Watasema: “Ni Allaah.”[7]

Aayah kama hizi ni nyingi katika Qur-aan. Yule mwenye kudai kwamba Tawhiyd ni kule kukubali juu ya uwepo wa Allaah au kukubali kwamba Allaah ndiye muumbaji na mwenye kuendesha ulimwengu na akatosheka juu ya sampuli hii, basi atakuwa hakutambua uhakika wa Tawhiyd ambayo Mitume walilingania kwayo. Amesimama katika dalili na akaacha kinachoonyeshewa dalili.

Miongoni mwa sifa za kipekee za ´ibaadah ni ukamilifu usiyofungamana kwa pande zake zote usiyokuwa na upungufu wowote ndani yake kwa njia zake zote. Hayo yanalazimisha ´ibaadah zote ziwe kwa ajili Yake pekee, kumuadhimisha, kumtukuza, tisho, maombi, kurejea, kutubia, utegemezi, kutakwa uokozi, upeo wa kujidhalilisha na upeo wa kupenda, yote hayo yanalazimika – kiakili, Kishari´ah na kimaumbile – yawe kwa ajili ya Allaah pekee na yakataa – kiakili, Kishari´ah na kimaumbile – kufanyiwa mwengine.

[1] 02:21-22

[2] 23:84-89

[3] 06:102

[4] 51:56

[5] 43:87

[6] 43:09

[7] 10:31

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 36-39
  • Imechapishwa: 06/02/2020