Nasaha zangu kwa ndugu zangu waislamu ni kwamba wasidanganyike na wale wanaodai uwalii mpaka kwanza wazipime hali zao kutokana na yale yaliyopokelewa katika maandiko juu ya sifa za mawalii wa Allaah. Shaykh (Rahimahu Allaah) ameashiria alama za mapenzi ya kumpenda Allaah kutokana na yale aliyotaja katika Aayah zifuatazo:

1 – Allaah (Ta´ala) amesema katika Aal ´Imraan:

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ

“Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni atakupendeni Allaah.”[1]

Aayah hii inaitwa ´Aayah ya mtihani`. Wako watu waliodai kumpenda Allaah ndipo Allaah akateremsha Aayah hii. Kwa hivyo yule anayedai kumpenda Allaah basi tutayaangalia matendo yake. Akiwa ni mwenye kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi ni mkweli. Vinginevyo ni mwongo.

2 – Allaah (Ta´ala) amesema katika al-Maaidah:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا مَن يَرْتَدَّ مِنكُمْ عَن دِينِهِ فَسَوْفَ يَأْتِي اللَّـهُ بِقَوْمٍ يُحِبُّهُمْ وَيُحِبُّونَهُ أَذِلَّةٍ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ أَعِزَّةٍ عَلَى الْكَافِرِينَ يُجَاهِدُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَلَا يَخَافُونَ لَوْمَةَ لَائِمٍ

”Enyi mlioamini! Yeyote atakayeritadi miongoni mwenu kutoka dini yake, basi Allaah atawaleta watu [badala yao] Atakaowapenda nao watampenda; wanyenyekevu kwa waumini, wenye nguvu juu ya makafiri; wanafanya jihaad katika njia ya Allaah na wala hawakhofu lawama ya mwenye kulaumu.”[2]

Amewasifu kwa sifa mbili ambazo ndio alama na athari ya mapenzi:

1 – Ni wanyenyekevu kwa wuamini. Kwa msemo mwingine ni kwamba hawawapigi vita, hawasimami dhidi yao wala hawawapachiki majina ya kuwabeza.

2 – Ni wenye nguvu juu ya makafiri na ni wenye kuwashinda.

3 – Wanafanya jihaad katika njia ya Allaah. Bi maana hutumia juhudi zao katika kupambana na maadui wa Allaah ili neno la Allaah liwe juu.

4 – Hawakhofu kwa ajili ya Allaah lawama za mwenye kulaumu. Akipatikana yeyote mwenye kuwalaumu kutokana na yale mambo ya dini waliyofanya basi hawaogopi lawama zake. Isitoshe hilo haliwazuii kutekeleza dini ya Allaah.

5 – Allaah (Ta´ala) amesema katika Yuunus:

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ

“Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hawana khofu juu yao na wala hawatohuzunika. Ambao wameamini na wakawa wanamcha.”[3]

Allaah (Ta´ala) amebainisha kuwa mawalii wa Allaah ni wale wenye kusifika kwa sifa hizi mbili:

1 – Imani.

2 – Kumcha Allaah.

Wana imani ndani ya moyo na wanamcha Allaah juu ya viungo vyao vya mwili.

Ambaye anajidai kuwa ni walii wa Allaah lakini asisifike na sifa mbili hizi basi ni mwongo.

[1] 03:31

[2] al-Maaidah 05:54

[3] 10:62-63

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 27/06/2021