16. Salafiyyuun tu ndio wawezao kupambana na ugaidi


Mfumo wa kutibu ugaidi na kinga dhidi ya maradhi haya ni ushauri wa Kiislamu na mwongofu ambao hakuna wengine wenye kuumairi isipokuwa tu wanachuoni Salafiyyuun wanaofuata mifumo ya kiutume. Ushauri wao umejengwa juu ya tabia, mawaidha na maelekezo ya Mitume na Manabii – watu ambao Allaah amewatuma ili kulingania na kuwafunza watu.

Kituo chao cha kuanza ni Wahy wa kimungu unaozipa uhai mioyo ili zisigonjweke, kuzituliza nyoyo ili zisichanganyikiwe na kupagawa. Isipokuwa tu wale walioghilibiwa na matamanio na wakaandikwa kama wapotevu kwenye Ubao uliohifadhiwa. Kuhusu wao, wanaguswa na Aayah ifuatayo:

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ ۚ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ

“Hakika wewe huwezi kumwongoza umtakaye, lakini Allaah ndiye amwongozaye amtakaye – Naye anawajua zaidi wenye kuongoka.”[1]

Pindi wasipowaidhika kwa mawaidha na vitabu, basi Allaah atawanufaisha kwa upanga wa haki kupitia mkononi mwa mtawala wa Kiislamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth ndefu:

“Mtaamrishana mema na kukatazana maovu, kumzuia mtenda dhambi na kumvuta katika haki. Vinginevyo Allaah atazigonganisha nyoyo zenu nyinyi kwa nyinyi au atakulaanini kama alivyowalaani.”[2]

Bila ya shaka jamii ina nafasi kubwa katika ulinzi na kupambana na maradhi ya ugaidi, lakini hilo halipelekei katika taathira nzuri ikiwa [jamii hiyo] haina maumbile yaliyosalimika na elimu ya Kiislamu ya kisawa.

Kwa kufupisha ni kwamba dawa pekee dhidi ya ugonjwa wa ugaidi katika miji ya Kiislamu ni Wahy wa kimungu ubaobebwa na kufikishwa na watu wenye kuuelewa na kujua namna utakavyofikishwa. Matabibu wake ni wale wanachuoni katika njia ya Mtume na wale watawala wachaji na baada ya hapo jamii, mdogo kwa mkubwa, ndani ya nchi na nje ya nchi, kwa mujibu wa yale yaliyotajwa punde tu:

مَن يَهْدِ اللَّـهُ فَهُوَ الْمُهْتَدِ ۖ وَمَن يُضْلِلْ فَلَن تَجِدَ لَهُ وَلِيًّا مُّرْشِدًا

“Ambaye Allaah amemwongoza, basi huyo ndiye kaongoka, na anayempotoa, basi hutompatia mlinzi wa kumuongoza.”[3]

[1] 28:56

[2] Ahmad (1/391), Abu Daawuud (4336), at-Tirmidhiy (3048) na Ibn Maajah (4006) kupitia kwa Abu ´Ubaydah bin ´Abdillaah bin Mas´uud kutoka kwa baba yake. Kuna maoni tofauti kama alisikia kitu kutoka kwake. Hadiyth ni nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy. Tazama ”Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” (1105).

[3] 18:17

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Irhaab, uk. 23-24
  • Imechapishwa: 14/04/2017