16. Njia ya nane: kusoma hima na historia ya Salaf

Miongoni mwa njia ya kuifikia elimu ni kusoma hima waliokuwa nayo Salaf katika masomo. Mwanafunzi anatakiwa kusoma vitabu na historia ya Salaf. Hakika katika historia yao kuna ya mambo ya kushangaza. Ninaapa kwa Allaah ya kwamba mwenye kusoma vitabu vya Salaf na akajua kile walichokuwa wanafanya katika kusoma, basi yatamkuwia mepesi yale [mazito] atayokutana nayo na atatambua kuwa si lolote si chochote.

Tumtazame Shu´bah (Rahimahu Allaah) ambaye amesafiri mwezi mzima kwa ajili ya kupata Hadiyth ambayo alikuwa nayo, lakini kuna mwingine alikuwa ameipokea kwa njia nyingine na hivyo akasafiri mwezi mzima kwa ajili ya kupata Hadiyth hii iliyopokelewa kwa njia nyingine[1].

Mwengine ni Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye alinunua ngamia na akasafiri kwenda nae Shaam mwendo wa mwezi mzima ili aweze kusikia Hadiyth moja tu kutoka kwa ´Abdullaah bin Unays ambayo hakuisikia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[2].

Imaam Ahmad, wakati alikuwa bado kijana mdogo, bali wakati alikuwa bado akingali ni mtoto mchanga, alikuwa akikimbilia kutoka nyumbani mwishoni mwa usiku ili aweze kufika katika mzunguko wa kielimu. Mama yake alikuwa akimshika nguo yake na kumwambia:

“[Baki huko] mpaka kupambazuke.”[3]

Tukisoma historia ya Salaf basi tutaona mambo ya ajabu sana.

[1] Tazama “Dhwu´afaa’ (02/191) ya al-´Aqiyl, “al-Qiraa´ khalf al-Imaam”, uk. 207-208 ya al-Bayhaqiy na wengineo

[2] al-Bukhaariy (01/174) katika Fath-ul-Baariy

[3] Tazama “Siyar A´laam-in-Nubalaa'” (11/306)

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Ilm wa Wasaaailuh wa Thimaaruh
  • Imechapishwa: 22/10/2016