16. Ni wajibu kwa muislamu kuchelea juu ya dini yake


Ni wajibu kwa muislamu kuogopa juu ya dini yake zaidi ya ambavyo anaogopa juu ya nafsi yake na mali yake. Aogope juu ya dini yake kwa kitu gani? Juu ya fitina na utata. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kutakuwa na fitina kama kipande cha usiku wenye giza. Mtu atafika asubuhi akiwa ni muumini na ikifika jioni tayari ameshakuwa kafiri na anafika jioni akiwa ni muumini na ikifika asubuhi tayari ameshakuwa kafiri. Anaiuza dini yake kwa sababu ya dunia.”[1]

Muislamu midhali bado yuko hai basi yuko khatari kutokana na fitina na kuritadi kutoka katika Uislamu. Ndio maana kiongozi wa Tawhiyd Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuomba Mola wake kwa kusema:

وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَن نَّعْبُدَ الْأَصْنَامَ  رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ

“Unikinge mimi na wanangu kuabudu masanamu.” Ee Mola wangu! Hakika hao wamepoteza wengi kati ya watu.” (an-Nahl 14:35-36)

Ibraahiym huyu ambaye aliyavunja masanamu kwa mkono wake na akaudhiwa kwa ajili hiyo mpaka akatupwa motoni anachelea juu ya nafsi yake asije kuritadi kutoka katika Tawhiyd na kuabudu masanamu. Kwa sababu wale walioyaabudu ni aina miongoni mwa watu, wana akili na uelewa. Lakini hata hivyo akili na uelewa wao haukuwafaa kitu na kuwazuia kuyaabudu masanamu. Ibraahiym (´alayhis-Salaam) pindi alipoona wengi ambao wameteleza na kufitinishwa kuyaabudu masanamu ndipo akachelea juu ya nafsi yake. Hivyo akamuomba Mola wake amthibitishe katika dini ya Tawhiyd na asiupotoshe moyo wake kama walivyopotea watu hawa. Kwani watu hawa ni watu kama yeye. Mtu hakuaminiwi juu yake fitina. Kwa ajili hii alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – naye ndiye mtu ambaye yuko na imani na Tawhiyd kamilifu zaidi – akichelea juu ya nafsi yake na hivyo akiomba kwa kusema:

“Ee Mwenye kuzipindua nyoyo! Uthibitishe moyo wangu katika dini Yako.” ´Aaishah ambaye ni mama wa waumini anamuuliza: “Ee Mtume wa Allaah! Hivi unachelea juu ya nafsi yako?” Anajibu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ee ´Aaishah! Ni kipi kitachoniaminisha ilihali nyoyo za waja ziko kati ya vidole viwili katika vidole vya Mwingi wa huruma?”[2]

Kwa ajili hiyo Ibraahiym na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam) walikuwa wakichelea juu ya dini zao na wakirejea kwa Allaah awaongoze dhidi ya yale waliyotumbukiaemo wengi katika viumbe. Wale ambao hali zao ziko chini kuliko wao wana haki zaidi ya kuogopa. Hivyo basi muislamu anatakiwa kuchelea juu ya dini yake, nafsi yake, shari ya walinganizi waovu, utata na fitina kukiwemo fitina ya matamanio na fitina ya utata. Mtu anapaswa kuogopa yote hayo.

Mtu akishaogopa basi anatakiwa kufuata zile sababu za usalama na ajiepushe na sababu za maangamivu. Ama kuogopa peke yake na hafuati zile sababu za  usalama na wala hajiepushi na zile sababu za maangamivu, khofu peke yake haitoshi. Ni lazima khofu iambatane na matendo ambayo itamlinda na fitina hii.

[1] Ameipokea Muslim (186)  na at-Tirmidhiy (2195) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

[2] Ameipokea Ahmad (24604), al-Aajurriy katika “ash-Shariy´ah” (733), an-Nasaa´iy (7290 na Ibn Abiy ´Aaswim (240). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy (Rahimahu Allaah).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 36-38
  • Imechapishwa: 26/06/2018