1- Muhammad al-Baqiyr amesema:

“al-Husayn bin ´Aliy alihiji hajj kumi kwa kutembelea mguu ilihali ngamia wake anatembea pembezoni naye.”

2- Watu bora ni wale wenye kunyenyekea ilihali wanaweza kujinyanyua, kuipa nyongo dunia ilihali wako na uwezo na waadilifu ilihali wanaweza kuadhibu. Mtu kamwe haachi kunyenyekea isipokuwa huingiwa na kiburi. Hakuna anayewadharau watu isipokuwa ni kwa sababu anajivuna. Mtu kujiona ndio ugonjwa wa akili yake. Sijaona mtu ambaye anamdharua aliye chini yake isipokuwa Allaah humdhalilisha kwa aliye juu yake.

4- Mwenye busara akimuona ambaye anamzidi umri, ananyenyekea mbele yake na kusema: “Alinitangulia kuwa muislamu.” Anapomuona ambaye ana umri mdogo kuliko yeye, hunyenyekea mbele yake na kusema: “Nina dhambi nyingi kuliko yeye.” Akimwona ambaye wako umri sawa, anamzingatia kama nduguye. Ni vipi mtu anaweza kumfanyia kiburi ndugu yake? Haifai mtu kumdharau mwengine.

5- Ibn ´Abbaas amesema:

“Lau mlima ungelishambulia mlima mwingine basi Allaah angelivunja ule mlima uliyoshambulia.”

6- Nuuh bin Qays ameeleza kuwa nduguye amesema:

“Qataadah amesema: “Sijawahi kamwe kusahau kitu.” Kisha akamwambia mtumwa wake: “Nipe viatu vyangu.” Ndipo yule mtumwa wake akamwambia: “Umevivaa miguuni mwako.”[1]

7- al-Fadhwl bin Muusa amesema:

“Maalik alikuwa akisahau, ndipo akamwambia mfanya kazi wake: “Ninunulie mtumwa na mpe jina jepesi ili nisilisahau.” Mfanya kazi akamnunulia na akamleta kwake na kusema: “Nimekununulia mtumwa na nimempa jina jepesi.” Akauliza: “Anaitwa nani?” Akamwambia: “Farqad.” Maalik akamtazama mtumwa yule na akasema: “Kaa chini, ee Waaqid!”

[1] ”Kinacholengwa ni kwamba amesahau kitu kisichosahaulika, jambo ambalo linathibitisha kuwa madai yake si ya sawa.” (Taaliki ya ”Rawdhwat-ul-´Uqalaa´, uk. 63)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 62-63
  • Imechapishwa: 06/02/2018