5- Kutilia umuhimu Sunnah za kinabii, kupupia kuzitendea kazi na kulingania katika jambo hilo

Hakika jambo lenye haki zaidi analoweza kufanya muislamu ni kujitahidi kufuata mapokezi ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuzifanyia kazi katika maisha yake kwa kiasi cha mtu anavoweza. Hilo ni kwa sababu lengo kuu analojaribu kulifikia muislamu ni kufikia uongofu utaomfikisha Peponi. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا

”Mkimtii basi mtaongoka.”[1]

وَاتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ

“Mfuateni ili mpate kuongoka.”[2]

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا

“Hakika mna kigezo chema kwa Mtume wa Allaah kwa yule mwenye kumtaraji Allaah na siku ya Mwisho na akamtaja Allaah kwa wingi.”[3]

Aayah hii ndio msingi mkuu katika kumuigiliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika maneno, vitendo, hali zake zote mpaka kutikisika na kutulizana kwake. Kiigizo hichi kizuri yule anayemfuata ni yule aliyeongozwa miongoni mwa wale wenye kutaraji kukutana na Allaah na siku ya Mwisho kutokana na ile imani alionayo, kumwogopa Allaah kutaraji thawabu Zake na kuogopa adhabu Yake, mambo yanayomfanya kumwigiliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Utukufu na hadhi ya muumini inapimwa kwa kule kumfuata kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kila ambavyo mtu atakuwa na bidii na ni mwenye kuchunga zaidi Sunnah, basi ndivo anavyokuwa na haki zaidi kupata ngazi za juu.

[1] 24:54

[2] 07:158

[3] 33:21

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Usuwl-ud-Da´wah as-Salafiyyah, uk. 47-48
  • Imechapishwa: 11/08/2020