16. Msingi wa saba: kuipenda familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)

Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kuwapenda watu wa familia ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhiwa sallam) na kuwafanya ni marafiki kwa kutendea kazi wasia wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

“Ninakukumbusheni Allaah juu ya watu wa nyumbani kwangu.”[1]

Miongoni mwa watu wa nyumbani kwake ni wakeze (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao ni mama wa waumini – Allaah awawie radhi wote. Allaah amesema baada ya kuwazungumzisha pale aliposema:

يَا نِسَاءَ النَّبِيِّ

“Enyi wake wa Nabii!”[2]

akazielekeza nasaha kwao na akawaahidi malipo makubwa:

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا

“Hakika si venginevyo Allaah anataka akuondosheeni maovu, enyi watu wa nyumbani kwa Mtume, na akutakaseni mtakaso barabara.” [3]

Kimsingi watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni wale ndugu zake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walengwa hapa ni wale wema peke yao. Kuhusiana na wale ndugu zake ambao si wema hawana haki yoyote. Mmoja katika hao ni ami yake Abu Lahab na mfano wake. Amesema (Ta´ala):

تَبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ

“Imeteketea mikono miwili ya Abu Lahab na ameteketea.”[4]

Kule kuwa na udugu na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) peke yake na kujinasibisha naye pasi na kunyooka katika dini hakumnufaishi mwenye kufanya hivo mbele ya Allaah na chochote. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Enyi Quraysh! Ziuzeni nafsi zenu! Hakika mimi sintokunufaisheni mbele ya Allaah na chochote. Ee ´Abbaas ami ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)! Sintokunufaisha mbele ya Allaah na chochote. Ee Swafiyyah shangazi yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)! Sintokunufaisha mbele ya Allaah na chochote. Ee Faatwimah binti ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)! Niombe katika mali utakacho! Hakika mimi sintokunufaisha mbele ya Allaah na chochote.”[5]

Wale nduguze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao ni wema wana haki juu yetu ya kutukuzwa, kupendwa na kuheshimiwa. Pamoja na hivyo haijuzu kwetu kupetuka mipaka kwao na tukajikurubisha kwao kwa kuwatekelezea kitu katika ´ibaadah au tukaamini ya kwamba wananufaisha au wanadhuru pasi na Allaah. Allaah (Subhaanah) anasema kumwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

قُلْ إِنِّي لَا أَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا رَشَدًا

“Sema: “Hakika mimi sikumilikieni dhara na wala uongofu.””[6]

قُل لَّا أَمْلِكُ لِنَفْسِي نَفْعًا وَلَا ضَرًّا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ ۚ وَلَوْ كُنتُ أَعْلَمُ الْغَيْبَ لَاسْتَكْثَرْتُ مِنَ الْخَيْرِ وَمَا مَسَّنِيَ السُّوءُ

“Sema: “Siimilikii nafsi yangu manufaa wala dhara yoyote isipokuwa atakavyo Allaah na lau ningekuwa najua ya ghaibu, basi bila shaka ningelijikithirishia ya kheri na wala lisingelinigusa ovu.”[7]

Vipi kwa mtu mwengine ikiwa hali ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) iko namna hii? Yale wanayoitakidi baadhi ya watu miongoni mwa wale wanaojinasibisha udugu na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni I´tiqaad batiili.

[1] Muslim (2408) na Ahmad (04/367)

[2] 33:32

[3] 33:33

[4] 111:01

[5] al-Bukhaariy (2602), Muslim (206), at-Tirmidhiy (3185), an-Nasaa´iy (3646) na Ahmad (06/350)

[6] 72:21

[7] 07:188

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Usuwl ´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 34-36
  • Imechapishwa: 12/05/2022