16. Malezi sahihi


Imani ina vipengele vitatu:

1 – Kuzungumza kwa ulimi.

2 – Kuamini ndani ya moyo.

3 – Vitendo vya viungo.

Haitoshi kipengele kimoja au viwili. Bali ni lazima kupatikane vipengele vyote vitatu.

Katika kitabu hiki na utangulizi wake mtunzi ametaja ´Aqiydah kwa jumla, ´ibaadah za wajibu na zilizopendekezwa, adabu na misingi ya Fiqh yenye kuenea. Lengo ni ili mtoto akulie juu ya utambuzi na uhakika wa imani kwa kifupi. Namna hii mtoto anatakiwa kufunzwa vitabu vifupivifupi. Vitabu vifupivifupi ndio ufunguo wa elimu. Ndio msingi. Kwa ajili hiyo ndio maana husemwa kwamba yule mwenye kunyimwa misingi atanyimwa pia kufika, nako ni kuifikia elimu yenye manufaa. Mwanafunzi anayeanza, mtoto au mkubwa, hatakiwi kuanza na vitabu vikubwavikubwa kama mfano wa “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy na Muslim, “al-Mughniy” na vitabu vya Siybuuyah. Mwanafunzi anayeanza anatakiwa kupelekwa hatua kwa hatua. Kuanza moja kwa moja na vitabu vikubwavikubwa na vilivyoingia kwa undani zaidi ni kuchoka kusikokuwa na faida. Mtu kama huyo ataishilia njiani na hatofaidika chochote. Kwa sababu anafuata njia isiyokuwa sahihi ya elimu. Amesema (Ta´ala):

وَلَيْسَ الْبِرُّ بِأَن تَأْتُوا الْبُيُوتَ مِن ظُهُورِهَا وَلَـٰكِنَّ الْبِرَّ مَنِ اتَّقَىٰ ۗ وَأْتُوا الْبُيُوتَ مِنْ أَبْوَابِهَا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

“Na si wema kuingia nyumba kwa nyuma yake, lakini wema ni kwa anayemcha Allaah, na ingieni majumbani kupitia milango yake. Na mcheni Allaah mpate kufaulu.”[1]

Mwanafunzi anayeanza anatakiwa kufunzwa mambo ya wajibu. Asifunzwe mambo ya matawi na ya upambanuzi. Mwanzoni anatakiwa kufunzwa mambo ya wajibu ya dini. Baadaye wanapovuka hatua hii ya mwanzoni, ndipo wafunzwe kwa kubobea ndani zaidi. Wabainishiwe maoni mbalimbali, dalili na maoni yaliyo na nguvu zaidi. Lakini haya yanakuwa baada ya kufunzwa misingi. Wanatakiwa kupelekwa hatua kwa hatua; waanzilishwe vitabu vifupivifupi, vitabu vya kati na kati na kisha mwishowe vitabu vikubwavikubwa. Namna hii ndivo inavosomwa elimu. Huu ndio mfumo wa maelezi sahihi.

[1] 2:189

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 19-20
  • Imechapishwa: 07/07/2021