16. Kujengea hoja kuingizwa kaburi la Mtume msikitini

Swali: Imepokelewa katika Hadiyth:

”Allaah awalaani watu waliofanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni mahali pa kuswalia.”

Ni jambo linatokea katika nchi nyingi za Kiislamu kuyafanya makaburi ya mawalii [kuwa ni mahali pa kuswalia]. Wakati tunapowakataza jambo hilo wanajengea hoja ya kwamba kaburi lake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) lipo ndani ya msikiti al-Madiynah al-Munawwarah, jambo ambalo linatuletea baadhi ya utatizi.

Jibu: Hapana shaka kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah awalaani mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni mahali pa kuswalia.”

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) akasema:

“Anatahadharisha yale waliyoyafanya.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim katika “as-Swahiyh” zao.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Tanabahini! Hakika wale waliokuwa kabla yenu walikuwa wakiyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa mahali pa kuswalia. Tanabahini! Msiyafanye makaburi kuwa mahali pa kuswalia. Hakika mimi nawakatazeni na hilo.”[2]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Hadiyth hii na nyenginezo zilizopokelewa zikiwa na maana kama hiyo zote ziko wazi kuonyesha kuwa ni haramu kuijengea misikiti juu ya makaburi, kuswali, kusoma Qur-aan karibu na makaburi na mfano wa hayo. Baadhi ya watu wanaweza kutatizika na mambo na wasitambue uhakika wa yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hivyo matokeo yake wakafanya watakayofanya katika kuijenga misikiti juu ya makaburi na kuifanya kuwa ni mahali pa kuswalia kwa sababu ya ujinga na uchache wa elimu.

Kuhusu yale yanayohusiana na kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuzikwa ndani ya msikiti. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alizikwa nyumbani kwa ´Aaishah. Kisha baadaye ukapanuliwa msikiti katika zama za al-Waliyd bin ´Abdil-Malik mwishoni mwa karne ya kwanza. Hapo ndipo chumba kikaingizwa ndani ya msikiti. Hili ni kosa la al-Waliyd alilofanya. Alikosolewa na baadhi ya waliokuwepo Madiynah kipindi hicho. Lakini hata hivyo haikukadiriwa kuyazingatia aliyokatazwa.

Kwa kufupisha ni kwamba kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) lilikuwa nyunbani kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) kisha ndio baadaye chumba kikaingizwa ndani ya msikiti kwa sababu ya kuupanua msikiti. Kwa hivyo hakuna hoja juu ya hilo.

Kitendo cha kiongozi wa waumini al-Waliyd bin ´Abdil-Malik alikosea katika jambo hilo wakati alipoiingiza ndani ya msikiti. Kwa hivyo haitakikani kwa yeyote kujengea hoja kitendo hichi. Yale yanayofanywa na watu hii leo ambapo wanayajengea makaburi na kuyafanya kuwa ni mahali pa kuswalia yote ni maovu yanayokwenda kinyume na mwongozo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kwa hivyo ni lazima kwa watawala kuyaondosha. Ni lazima kwa mtawala yeyote miongoni mwa watawala wa waislamu kuindosha misikiti hii iliyojengwa juu ya makaburi na afuate Sunnah. Makaburi jangwani yawe waziwazi na kusiwepo juu yake majengo, makuba, misikiti wala kitu kingine. Hivo ndivo yalivyokuwa makaburi wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) al-Baqiy´ yalikuwa waziwazi hayakuwa na kitu. Vivyo hivyo makaburi ya mashahidi wa Uhud juu yake hayakuwa na kitu.

Kwa kumalizia ni kwamba haya ndio yaliyowekwa katika Shari´ah. Makaburi yanatakiwa yawe waziwazi na kusiwe juu yake na jengo, kama hali ilivyokuwa zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na katika zama za Salaf. Kuhusu yale yaliyozuliwa na watu katika kujenga ni Bid´ah na maovu. Haijuzu kuyakubali wala kuyaigiliza. Shirki ilizuka kwa sababu hii wakati watu wasiokuwa na elimu na wajinga walipoyakuta makaburi  yaliyojengwa juu yake misikiti, makuba yenye kutukuzwa, yaliyovishwa kitambara na yaliyotiwa manukato ndipo wakafikiria kuwa yanatatua haja zao, wanawaponya wagonjwa wao na kuwanufaisha. Matokeo yake wakayaomba, wakayataka uokozi na kuyawekea nadhiri. Shirki ikatokea namna hiyo. Tunaomba ulinzi kwa Allaah kutokamana na sababu zinazopelekea katika hayo. Kuchupa mpaka katika makaburi yote ni shari. Kwa ajili hiyo amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Jihadharini na kuchupa mpaka katika dini. Hakika si venginevyo wamechupa mpaka waliokuwa kabla yenu kule kuchupa mpaka katika dini.”[3]

Tunamuomba Allaah usalama na afya.

[1] al-Bukhaariy (436) na Muslim (529).

[2] Muslim (532).

[3] Ahmad (3238), an-Nasaa´iy (3075) na Ibn Maajah (3029).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 71-72
  • Imechapishwa: 03/05/2022