Swali 16: Pamoja na kwamba makundi na walinganizi wanaolingania katika dini ya Allaah ni wengi hii leo lakini hata hivyo uitikiaji ni mdogo. Ni ipi sababu ya hilo?

Jibu: Mosi sisi hatushaji´ishi makundi mengi katika ulinganizi na mengineyo. Sisi tunataka kundi moja tu la kweli linalolingania kwa Allaah kwa ujuzi. Wingi wa makundi na wingi wa mifumo ni jambo linalosababisha tu udhaifu na magomvi. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ

“Na wala msizozane, mtavunjikwa moyo na zikatoweka nguvu zenu.”[1]

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ تَفَرَّقُوا وَاخْتَلَفُوا

“Na wala msiwe kama wale waliofarikiana na wakakhitilafiana.”[2]

Sisi tunataka kundi limoja tu linalofuata mfumo sahihi na ulinganizi sahihi.  Hata kama litakuwa katika miji mbalimbali wana marejeo moja, wanarejea baadhi kwa wengine na kusaidiana kati yao. Wingi wa makundi ambayo hayakujengwa juu ya mfumo mmoja hatimaye huisha na tofauti.

Pili ni kwamba haina shaka yoyote kwamba mlinganizi kumtakasia nia Allaah humuathiri yule mlinganiwa. Ikiwa mlinganizi ni mwenye kumtakasia nia Allaah na analingania katika mfumo sahihi kwa utambuzi na ujuzi, basi itamuathiri yule mlinganiwa. Lakini asipokuwa ni mwenye kumtakasia nia Allaah na badala yake analingania katika nafsi yake mwenyewe, analingania katika chama chake, katika kundi lililopinda au ushabiki – hata kama yatajiita kwa jina la Uislamu – haya hayanufaishi lolote na hayana lolote kuhusiana na kulingania katika Uislamu.

Vilevile mlinganizi akiwalingania watu katika Qur-aan na Sunnah lakini hatendei kazi yale anayoyalingania kwayo, hili pia hufanya watu wakamkimbia. Allaah anajua yaliyomo mioyoni na anajua kile anachofanya kila mmoja pahali popote pale. Ikiwa mtu anamuasi Allaah wakati anapokuwa peke yake na anawalingania watu katika kheri pale anapokuwa pamoja nao, hili halitoathiri chochote na wala hatokubaliwa. Kwa sababu Allaah hakubariki ulinganizi wake. Watazame walinganizi waliokuwa na imani takasifu na namna linganizi zao zilivyobeba matunda. Walikuwa peke yao na walikuwa na wapinzani. Mfano wa watu hawa ni Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah, Imaam Ibn-ul-Qayyim al-Jawziy na Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab na  wengineo. Upande mwingine tazama walinganizi wengi na makundi mengi yote haya yaliyopo hii leo na jinsi athari yao na manufaa yao ni madogo kabisa, hivyo mtakuja kujua kuwa kinachozingatiwa ni ubora na si wingi.

[1] 08:46

[2] 03:105

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 41-43
  • Imechapishwa: 31/05/2023
  • mkusanyaji: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy