16. Je, Salaf walikuwa ni wenye kupatia au wenye kukosea?

73- Imethibiti kupitia Qur-aan, Sunnah na maafikiano kwamba ni wajibu kuwafuata Salaf. Hata akili inafahamisha hivo. Salaf ima walikuwa ni wenye kupatia au wenye kukosea. Kama walikuwa ni wenye kupatia basi ni w ajibu kufuata yale ya sawa na ni haramu kufuata jambo la makosa katika ´Aqiydah. Jengine ni kwamba kama walikuwa ni wenye kupatia basi walikuwa juu ya njia iliyonyooka. Yule mwenye kwenda kinyume nao ni mwenye kufuata njia ya shaytwaan inayoelekeza katika njia ya Motoni. Allaah (Ta´ala) ameamrisha kufuata njia Yake na amekataza kufuata vijia vyenginevyo. Amesema:

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Kwamba hii ni njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni na wala msifuate njia za vichochoro nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo alivyokuusieni kwayo mpate kumcha.”[1]

74- Akidai mwenye kudai kwamba walikuwa ni wenye kukosea, basi atakuwa ameutukana Uislamu wote. Kwa sababu kama waliweza kukosea katika jambo hili basi wangeliweza vilevile kukosea katika Uislamu mzima. Hivyo haitotakiwa kuyapokea mapokezi waliyopokea. Hivyo haitoweza kuthibitishwa miujiza ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) waliyopokea. Matokeo yake mapokezi yanabatilika na Shari´ah inaondoka. Hiki ni kitu ambacho hakitakiwi kusemwa na muislamu wala kukiamini. Ima Salaf walikuwa ni wenye kujua ni vipi maandiko haya yanatakiwa kufasiriwa au walikuwa hawajui. Kama walikuwa hawajui basi mtu anaweza kujiuliza sisi tulijua vipi. Na kama walijua lakini hata hivyo wakanyamaza basi na sisi vilevile tunatakiwa kunyamaza. Kwani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye mtangu wetu sote ambaye hakufasiri Aayah na Hadiyth hizi zinazozungumzia sifa. Yeye ni hoja ya Allaah kwa viumbe wote. Ni wajibu kwao kumfuata na imeharamishwa kwao kwenda kinyume naye. Allaah ameshuhudia kwamba yuko katika njia iliyonyooka, anaelekeza kwayo, kwamba wale wenye kumfuata wanapendwa na Allaah na wale wenye kumuasi wamemuasi Allaah:

وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا

“Yule mwenye kumuasi Allaah na Mtume wake, basi kwa hakika amepotoka upotevu wa wazi kabisa.”[2]

وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَتَعَدَّ حُدُودَهُ يُدْخِلْهُ نَارًا خَالِدًا فِيهَا وَلَهُ عَذَابٌ مُّهِينٌ

“Na yeyote atakayemuasi Allaah na Mtume Wake na akavuka mipaka Yake atamwingiza Motoni, ni mwenye kudumu humo na atapata adhabu ya kutweza.”[3]

[1] 06:153

[2] 33:36

[3] 04:14

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ut-Ta’wiyl, uk. 33-34
  • Imechapishwa: 19/12/2018