1- Mwenye kulala mchana mzima swawm yake ni sahihi. Kwani kulala hakuondoshi hisia. Mwenye kuzimia mchana mzima atatakiwa kuilipa siku yake hiyo. Kwa sababu ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia na kuzimia kunaondosha kabisa hisia. Ni lazima aweke nia kutokana na ujumla wa maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Hakika kila kitendo kinategemea na nia na kila mmoja atalipwa kwa kile alichonuia.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

2- Mfungaji akiota mchana wakati wa funga yake, basi tatakiwa kuoga na swawm yake ni sahihi. Hilo halimdhuru. Kwa sababu hakufanya kwa kupenda wala kutaka kwake. Allaah (Ta´ala) amesema:

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

”Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.”[1]

3- Mwenye kufunga akiamka hali ya kuwa na janaba swawm yake ni sahihi. Alfajiri ikimpambazukia na bado  yuko na janaba ya jimaa au akaota na asiwahi kuoga isipokuwa baada ya kuchomoza kwa alfajiri, atatakiwa kujizuia na chakula, kinywaji na vifunguzi vyengine kwa kuweka nia kabla ya kupambazuka kwa alfajiri. Hayo ni kutokana na yale yaliyothibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Aaishah na Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhumaa):

“Alfajiri ilikuwa ikimkuta naye yuko na janaba kutoka kwa mkewe. Kisha anaoga na kufunga.”[2]

Haya yanayofahamishwa na Hadiyth ndio maoni ya sawa wanayoona wanachuoni wengi. Wapo baadhi ya Taabi´uun wenye kuona kuwa swawm yake si sahihi. Baadaye tofauti ilikuja kuondoka kwa kujirejea kutoka katika maoni yao na hatimaye maafikiano yakatulizana juu ya yale yenye kufahamishwa na Hadiyth: nayo ni kusihi kwa funga ya aliyepatwa na janaba[3].

4- Kadhalika inamuhusu mwenye hedhi na damu ya uzazi itapokatika damu yao na wasiwahi kuoga isipokuwa baada ya kupambazuka kwa alfajiri, funga zao ni sahihi.

[1] 02:286

[2] al-Bukhaariy (1926) na Muslim (1109).

[3] Tazama ”Fath-ul-Baariy” (04/147) na ”Sharh-un-Nawawiy ´alaa Muslim” (07/222).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswaru fiy Ahkaam-is-Swiyaam, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 23/05/2019