16. Hukumu ya swalah ya ´Iyd na fadhila za siku sita za swawm ya Shawwaal

Ndugu muislamu! Jifunze baadhi ya hukumu muhimu unazotakiwa kuzijua zinazohusiana na mwezi huu mtukufu.

1 – Swalah ya ´Iyd

Kwa mujibu wa wanachuoni wengi swalah ya ´Iyd ni faradhi kwa baadhi ya waislamu. Inajuzu kwa baadhi kutoiswali. Hata hivyo imependekezwa kuihudhuria na mtu kushirikiana na ndugu zake waislamu. Ni Sunnah iliyokokotezwa isiyotakikana kuachwa isipokuwa kwa kuwepo udhuru wa Kishari´ah.

Baadhi ya wanachuoni wanaonelea kuwa ni lazima kwa waislamu wote kuiswali kama swalah ya Ijumaa. Wanaume wote katika mji na ambao wana majukumu juu ya matendo yao ni lazima waiswali. Maoni haya ndio yanaonekana kuwa dalili yenye nguvu na ilio karibu zaidi na usawa.

Ni Sunnah kwa wanawake kuihudhuria. Lakini wanatakiwa kuzingatia kujisitiri vizuri na kutojitia manukato. Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim ya kwamba Umm ´Atwiyyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametuamrisha kuwatoa nje siku ya ´Iyd mbili wanawake vijana ambao ndio karibuni wametoka kukomaa, wanawake wenye hedhi na mabikira. Kuhusiana na wanawake wenye hedhi, wajitenge mbali na kuswali.”[1]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Ee Mtume wa Allaah! Mmoja wetu hana Jilbaab ya kutoka nayo?” Akasema: “Dada yake ampe moja katika Jilbaab zake.””[2]

Ni jambo lisilo na shaka ya kwamba haya yanafahamisha kuwa imekokotezwa kwa wanawake kutoka na kuswali swalah za ´Iyd na washiriki kheri na du´aa ya waislamu.

Lililo Sunnah kwa anayefika mahala pa kuswalia swalah ya ´Iyd au swalah ya mvua akae moja kwa moja na wala asiswali Rakaa´ mbili za Sunnah kwanza. Kutokana na ninavyojua kitu kama hicho hakikupokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum). Isipokuwa tu ikiwa inaswaliwa msikitini. Katika hali hii atatakiwa kuswali Rakaa´ mbili za Sunnah kutokana na jumla ya maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mmoja wenu atapoingia msikitini asikae mpaka kwanza aswali Rakaa´ mbili.”[3]

Kwa ambaye amekaa na kusubiri swalah ya ´Iyd imewekwa katika Shari´ah akithirishe kusema “Laa ilaaha illa Allaah” na “Allaahu Akbar”. Ni nembo ya siku hiyo. Ni Sunnah kwa wote waliyoko ndani ya msikiti na nje ya msikiti mpaka Khutbah itapoisha. Ni sawa vilevile kujishughulisha na kusoma Qur-aan.

Napendelea kuweka wazi kwamba asli Takbiyr inatakiwa kutamkwa usiku wa ´Iyd na kabla ya swalah ya ´Iyd pamoja vilevile na yale masiku kumi ya mwanzo ya Dhul-Hijjah na masiku ya Tashriyq. Imewekwa katika Shari´ah kwenye masiku haya matukufu. Ndani yake mna fadhila tele kutokana na maneno ya Allaah (Ta´ala) juu ya Takbiyr katika mnasaba wa ´Iyd baada ya Ramadhaan:

وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

“… na ili mkamilishe idadi na ili mumkabiri Allaah kwa kuwa amekuongozeni na mpate kushukuru.”[4]

Allaah (Ta´ala) amesema pia kuhusu yale masiku kumi ya mwanzo ya Dhul-Hijjah na masiku ya Tashriyq:

لِّيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ ۖ فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْبَائِسَ الْفَقِيرَ

“… ili washuhudie manufaa yao na walitaje Jina la Allaah katika siku maalumu kwa yale aliyowaruzuku kati ya wanyama wenye miguu minne wa mifugo. Basi kuleni humo na lisheni mwenye shida fakiri.”[5]

Allaah (´Azza wa Jall) amesema vilevile:

وَاذْكُرُوا اللَّـهَ فِي أَيَّامٍ مَّعْدُودَاتٍ

“Mdhukuruni Allaah katika siku za kuhesabika.”[6]

Katika masiku haya maalum na yaliyotengwa imewekwa katika Shari´ah kumdhukuru Allaah kwa Takbiyr ambazo hazikufungamana na zilizofungamana. Ni jambo lina asli katika Sunnah twaharifu na matendo ya Salaf. Njia ya Takbiyr iliyowekwa katika Shari´ah ni kila muislamu kusema “Allaahu Akbar” kivyake. Anatakiwa kunyanyua sauti yake kiasi cha kwamba wengine waweze kumsikia ili wamuige na wadhukuru kupitia yeye. Kuhusu Takbiyr za kwa pamoja na zilizozuliwa, ni watu wasiopungua wawili wanyanyue sauti zao za Takbiyr kwa njia ya kwamba wanaanza na kumaliza kwa pamoja na wanafanya hivo kwa sauti ya pamoja na kwa njia maalum. Kitendo hichi hakina asli wala hakina dalili. Ni uzushi. Allaah hakuteremsha dalili yoyote juu ya hilo.

´Iyd ikiangukia siku ya Ijumaa ambaye ameswali swalah ya ´Iyd ana khiyari ya kuswali swalah ya Ijumaa au Dhuhr. Imethibiti kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Leo zimekutana sikukuu mbili. Aliyeswali ´Iyd hahitajii kuswali Ijumaa.”[7]

 Lakini hatakiwi kuacha kuswali Dhuhr. Lililo bora ni yeye kuswali swalah ya Ijumaa pamoja na wengine. Iwapo hatoswali swalah ya Ijumaa anatakiwa badala yake kuswali Dhuhr.

Kuhusu imamu anatakiwa kuswali swalah ya Ijumaa pamoja na wale waliohudhuria wakiwa hawapungui watu watatu pamoja na imamu. Endapo hakutohudhuria isipokuwa mtu mmoja tu ataswali Dhuhr pamoja naye.

Ni sawa kwa muislamu kumwambia ndugu yake siku ya ´Iyd au siku nyengine:

“Allaah atukubalie sisi na nyinyi matendo yetu mema.”

Sijui dalili yoyote juu ya hilo. Inahusiana tu na muumini kuwaombea nduguze du´aa nzuri kutokana na dalili nyingi juu ya hilo.

2 – Fadhila za swawm siku sita za Shawwaal

Swawm ya siku sita za Shawwaal ni Sunnah iliyothibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Imethibiti ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayefunga Ramadhaan kisha akaifuatisha na kufunga siku sita za Shawwaal, ni kama kufunga mwaka mzima.”[8]

Siku sita hizi hazikutengwa wakati maalum katika mwezi. Muumini ana khiyari kuzifunga atapotaka katika mwezi. Akitaka anaweza kuzifunga mwanzoni wa mwezi, katikati ya mwezi au mwishoni wa mwezi. Akitaka anaweza kuzifunga kwa kuziachanisha na akitaka anaweza kuzifunga kwa kuzifululiza. Kuna njia nyingi na himdi zote ni za Allaah. Hata hivyo lililo bora ni yeye kukimbilia kuzifunga mwanzoni mwa mwezi. Kwa sababu ni njia moja wapo ya kukimbilia matendo ya kheri. Kitendo hicho sio wajibu juu yake. Anaweza kuziacha katika mwaka wowote. Lakini kilicho bora na kamilifu zaidi ni kuendelea kuzifunga. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kitendo kinachopendwa zaidi na Allaah ni kile chenye kudumu ijapokuwa kitakuwa kichache.”[9]

Kuhusu mtu ambaye juu yake ana masiku yaliyompita ya Ramadhaan, anapaswa kuyafunga kwanza kabla ya kuanza kufunga swawm ya Sunnah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayefunga Ramadhaan kisha akaifuatisha na kufunga siku sita za Shawwaal, ni kama kufunga mwaka mzima.”

Atayefunga masiku sita kabla ya kutimiza Ramadhaan hakuifuatisha Ramadhaan yote. Ni faradhi kulipa yale masiku yaliyompita mtu na kufunga yale masiku sita ni Sunnah peke yake. Faradhi ndio inayopewa kipaumbele kabla ya Sunnah.

Ee waislamu! Kimbilieni kumcha Allaah (´Azza wa Jall) na kutafuta radhi Zake. Pambaneni na nafsi zenu juu ya kumcha Allaah (´Azza wa Jall) na hakikisheni daima mnatubia kikweli juu ya madhambi yote. Yapigeni vita matamanio, shaytwaan na nafsi yenye kuamrisha maovu. Ipupieni Nyumba ya Aakhirah. Mdhalilikieni Mola Wenu (´Azza wa Jall). Kithirisheni kumuomba du´aa na kumdhukuru kwa wingi na kumuomba msamaha. Ataziitikia du´aa zenu, kuzitengeneza hali zenu, kuwafanyia wepesi mambo yenu, kuwatunuku fadhila Zake, kuwasalimisheni na majanga yote na kuwalindeni na njama za maadui wenu na kila baya duniani na Aakhirah. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَالَّذِينَ جَاهَدُوا فِينَا لَنَهْدِيَنَّهُمْ سُبُلَنَا ۚ وَإِنَّ اللَّـهَ لَمَعَ الْمُحْسِنِينَ

“Na wale waliofanya juhudi kwa ajili Yetu, bila shaka Tutawaongoza njia Zetu. Hakika Allaah yu pamoja na wafanyao wema.”[10]

وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا ۚ يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا

“Allaah amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi – kama alivyowafanya makhalifa wale waliokuwa kabla yao – na atawamakinishia dini yao aliyowaridhia na atawabadilishia amani badala ya khofu yao – [kwa sharti] wananiabudu Mimi na hawanishirikishi na chochote.”[11]

وَإِن تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا لَا يَضُرُّكُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ

“Mkisubiri na mkaogopa haitokudhuruni chochote katika hila zao. Hakika Allaah ni mwenye kuyazunguka yote wayatendayo.”[12]

إِنَّ لِلْمُتَّقِينَ عِندَ رَبِّهِمْ جَنَّاتِ النَّعِيمِ

“Hakika wachaji Allaah watapata kwa Mola wao mabustani ya neema.”[13]

Ni jambo zuri kabisa hii leo mtu akajikurubisha kwa Allaah kwa kuwahurumia mafukara na wahitaji na kuwatendea wema. Hakika swadaqah ni miongoni mwa matendo makuu ambayo kwayo Allaah anazuia matatizo na kutunuku rehema. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَأَنفِقُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَلَا تُلْقُوا بِأَيْدِيكُمْ إِلَى التَّهْلُكَةِ ۛ وَأَحْسِنُوا ۛ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ

“Toeni katika njia ya Allaah wala msijitupe kwa mikono yenu katika maangamizi. Na fanyeni wema – Hakika Allaah anapenda wafanyao wema.”[14]

إِنَّ رَحْمَتَ اللَّـهِ قَرِيبٌ مِّنَ الْمُحْسِنِينَ

“Hakika Rahmah ya Allaah iko karibu na wafanyao wema.”[15]

وَأَن تَصَدَّقُواْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Mkitoa swadaqah basi ni kheri kwenu – mkiwa mnajua.”[16]

آمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَأَنفِقُوا مِمَّا جَعَلَكُم مُّسْتَخْلَفِينَ فِيهِ ۖفَالَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَأَنفَقُوا لَهُمْ أَجْرٌ كَبِيرٌ

“Muaminini Allaah na Mtume Wake na toeni kutokana na yale aliyokurithisheni; basi wale walioamini miongoni mwenu na wakatoa watapata ujira mkubwa.”[17]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swadaqah inafuta madhambi kama jinsi maji yanazima moto. Hali kadhalika swawm ya mtu usiku.”

Kisha akasoma:

تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ خَوْفًا وَطَمَعًا وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Mbavu zao zinatengana na vitanda wanamuomba Mola wao kwa khofu na matumaini na katika yale tuliyowaruzuku wanatoa. Basi nafsi yoyote haijui yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho. Ni malipo kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.”[18]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwingi wa Rahmah anawarehemu wenye huruma. Warehemu walio juu ya ardhi atakurehemuni Aliye juu ya mbingu.”[19]

Vilevile (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Asiyerehemu harehemiwi.”[20]

Tunamuomba Allaah azitengeneze hali za waislamu wote, azijaze nyoyo zao uchaji Allaah na awatengeneze viongozi wao na awafanye wote waweze kutubia kikweli kutokamana na madhambi yao na wawe na msimamo washikamane na Shari´ah ya Allaah (´Azza wa Jall) katika mambo yote. Tunamuomba Allaah awalinde kutokamana na njama za maadui wao. Hakika Yeye juu ya kila kitu ni muweza.

Swalah na amani zimwendee mja na Mtume Wake Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake.

[1] al-Bukhaariy (324) na Muslim (890).

[2] Muslim (890).

[3] al-Bukhaariy (1167) na Muslim (714).

[4] 02:185

[5] 22:28

[6] 02:203

[7] Abu Daawuud (1073) na Ibn Maajah (1311). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Abiy Daawuud” (948).

[8] Muslim (1164).

[9] al-Bukhaariy (5862) na Muslim (782).

[10] 29:69

[11] 24:55

[12] 03:120

[13] 68:34

[14] 02:195

[15] 07:56

[16] 02:280

[17] 57:07

[18] 32:16-17 Ibn Maajah (3973) na Ahmad (22069). Swahiyh kwa njia zingine kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (2866).

[19] Abu Daawuud (4941), at-Tirmidhiy (1924) na Ahmad (6494). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (3522).

[20] al-Bukhaariy (5997) na Muslim (2318).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mufiyd fiy Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 59-62
  • Imechapishwa: 02/04/2022