16. Elimu na matendo ni mambo mawili yenye kwenda sambamba


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mlango: Elimu kabla ya kauli na kitendo.

MAELEZO

Uwekaji mlango wa al-Bukhaariy unazingatiwa ni kama kanuni ya ki-Fiqh na ya kielimu. Kwa sababu amepita kutokana na yale aliyoyafahamu kutoka katika Qur-aan tukufu au kutoka katika Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ndipo akaweka mlango kama huu unaosema:

“Mlango: Elimu kabla ya kauli na kitendo.”

Ameyachukua hayo kutoka katika maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ

 “Basi elewa kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako.”[1]

Ameanza sehemu hii kwa kile alichoanza kwacho Allaah (´Azza wa Jall) katika amri hii iliyobarikiwa kwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Ummah wake ni wenye kufuata katika jambo hilo. Allaah amemwamrisha elimu kwanza. Hilo ni kwa sababu kila ´ibaadah inayofanywa bila ya elimu Allaah haipi uzito wowote. Bali ni lazima matendo yatanguliwe kwanza na elimu ili msomi awe juu ya ujuzi juu ya jambo lake.

Tumeshatangulia kusema kwamba elimu na matendo ni mambo mawili yenye kwenda sambamba na kwamba mwenye kukusanya kati ya viwili hivyo ameongozwa katika njia ilionyooka, kwamba mwenye kujua na asitende ameshika njia ya wale walioghadhibikiwa, kwamba mwenye kufanya matendo bila ya elimu – bali anatenda kwa ujinga na makosa – ameshika njia ya wale waliopotea. Hizi ni kanuni zinazotambulika vyema katika Uislamu. Katika maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ

 “Basi elewa kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah.”

inapendeza kwa mlinganizi na mwalimu asimame katika neno hili la Ikhlaasw ambalo ni “Laa ilaaha illa Allaah” ili afunze nguzo zake kwanza, sharti zake na haki zake na mambo yenye kulifanya likakamilika kwa kiasi cha uwezo wa mtu.

[1] 47:19

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Twariyqal-Usuwl ilaa idhwaah-ith-Thalaat-il-Usuwl, uk. 34-35
  • Imechapishwa: 25/11/2021