Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

11- Yuhai na hafi.

MAELEZO

Uhai Wake ni kamilifu na hauingiliwi na upungufu wala ulalaji:

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ

“Allaah, hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, Aliyehai daima, msimamizi wa kila kitu. Haumchukui usingizi wala kulala.”[1]

وَتَوَكَّلْ عَلَى الْحَيِّ الَّذِي لَا يَمُوتُ وَسَبِّحْ بِحَمْدِهِ

”Mtegemee Aliye hai ambaye hafi na tukuza kwa himdi Zake.”[2]

Amejikanushia Mwenyewe kushikwa na usingizi na kulala. Amejikanushia kufa kwa sababu uhai Wake (Subhaanah) ni kamilifu. Ulalaji, usingizi na kufa ni kasoro katika uhai. Sifa kama hizo ni za viumbe. Uhai wa viumbe ni wenye kasoro kwa sababu unashikwa na ulalaji na uchovu. Ulalaji ni sifa kamilifu kwa viumbe, kasoro kwa Allaah. Kiumbe asiyepata usingizi afya yake inazorota. Hii ni dalili inayofahamisha tofauti kati ya sifa za Muumbaji na sifa za viumbe. Allaah yuhai, msimamia kila kitu. Uhai Wake ni kamilifu na usimamizi Wake ni mkubwa kabisa.

[1] 02:255

[2] 25:58

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 37-38
  • Imechapishwa: 12/09/2019