158. Mwisho wa “Sharh Thalaath-il-Usuwl”


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Hii ndio maana ya “hapana mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah”.

Katika Hadiyth:

“Kichwa cha mambo ni Uislamu, nguzo yake ni swalah na Jihaad katika njia ya Allaah ndio nundu yake ya juu.”[1]

MAELEZO

Hii ndio maana… – Bi maana kukufuru Twaaghuut na kumwamini Allaah.

Uislamu maana yake ni kujisalimisha kwa Allaah kwa Tawhiyd, kunyenyekea Kwake kwa kumtii na kujitenga na shirki na washirikina. Hiki ndio kichwa cha mambo ya dini. Shahaadah mbili ndio kichwa cha Uislamu na pia ndio msingi wa Uislamu. Mtu haingii ndani ya Uislamu isipokuwa kwa kuzileta shahaadah mbili kwa kuzitamka, kiziitakidi, kuzitendea kazi na kuziamini. Mtu hawi muislamu kwa njia nyingine isipokuwa hiyo. Dini imefananishwa na mwili ulio na kichwa. Kinapokatwa kichwa au kusiwe kuna kichwa basi hakubaki uhai. Vivyo hivyo bila ya Tawhiyd hakuna dini yoyote. Kwa sababu ndio kichwa ambacho kikikatwa au kikaondoshwa basi umeondoka uhai na mwili umeharibika. Nguzo yake ambayo imesimama juu yake ni swalah.

Uislamu hausimami bila ya nguzo. Ni kama mfano wa nyumba isipokuwa na msingi ambao inasimama juu yake basi haiwezi kusimama. Nyumba haisimami isipokuwa kwa nguzo. Kukikosekana nguzo basi nyumba haisimami. Vivyo hivyo swalah ikikosekana basi Uislamu hausimami. Kwa ajili hiyo wanachuoni wamesema kuwa mwenye kuacha swalah kwa uvivu anakufuru kutokana na maoni yenye nguvu ijapokuwa anakubali uwajibu wake. Kwa sababu hakuna faida ya kukubali uwajibu pasi na kuitendea kazi. Hakuna faida kutokana na hilo. Kwa ajili hiyo wahakiki katika wanachuoni wamemhukumu ukafiri yule mwenye kuacha swalah kwa makusudi ingawa ni mwenye kutambua uwajibu wake. Kuhusu mwenye kukanusha uwajibu wake huyo ni kafiri kwa maafikiano ya waislamu.

Jihaad katika njia ya Allaah… – Nundu ni dini. Jihaad ni alama ya dalili ya Uislamu. Kunapokuweko jihaad katika njia ya Allaah hiyo ni dalili inayoonyesha nguvu ya Uislamu. Kwa sababu jihaad haiwi isipokuwa kutokana na nguvu ya imani na nguvu ya kiuchumi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefanya dini ni kwa mambo matatu: kichwa, nguzo na nundu. Hakuna uwepo wa dini kabisa kwa kukosekana kwa kichwa. Ambaye hahakiki kichwa, ambayo ndio Tawhiyd, hana dini yoyote. Ambaye haswali dini haisimami kwake hata kama atatamka shahaadah kwa sababu anahitaji nguzo ambayo dini itasimama juu yake. Nguzo hiyo haipatikani isipokuwa kwa kuswali. Kukikosekana jihaad basi inakosekana nguvu ya Uislamu na matokeo yake Uislamu unakuwa mnyonge na waislamu wanakuwa wanyonge. Hakuna nguvu ya Uislamu na kwa waislamu isipokuwa kwa kupambana jihaad katika njia ya Allaah (´Azza wa Jall). Hiyo ndio alama ya nguvu na kukosekana kwake ni alama ya udhaifu. Hivi ndio namna Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyofananisha mambo haya matatu kwa nisba ya dini: kichwa, nguzo na nundu. Ni kama ambavo ngamia inapokuwa na nundu ni dalili inayojulisha kuwa ni ngamia mwenye nguvu na asipokuwa na nundu anajulisha kuwa ni mnyonge na dhaifu. Kadhalika waislamu hii leo ni wanyonge ulimwenguni. Kwa ajili hii imepokelewa katika Hadiyth:

“Mtakapouziana kwa aina ya ribaa, mkashika mikia ya ng’ombe, mkaridhia kulima na mkaacha jihaad, basi Allaah atawasalitisha udhalili ambao hatauondoa mpaka mrudi katika dini yenu.”[2]

Kuacha jihaad ni unyonge na udhaifu kwa waislamu na kuweko kwake ni dalili ya nguvu kama ilivyo nundu kwa wanyama.

Allaah  ndiye mjuzi zaidi. Swalah na salamu zimwendeee Mtume wetu Muhammad.

Hapa ndipo mwisho wa maelezo ya kitabu hichi kilichobarikiwa ”Thalaath-ul-Usuwl”.

[1] at-Tirmidhiy (2616) na an-Nasaa´iy (10/214-215) (11330).

[2] Abu Daawuud (3462).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 309-310
  • Imechapishwa: 25/02/2021