157. Hakuna tofauti kati mwenye kufanya mzaha, anayekusudia au mwenye kuogopa II

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

… na mwenye kuogopa…

MAELEZO

Mwenye kusema neno na kufuru au akafanya kitendo na kufuru kwa sababu ya kuwaogopa makafiri. Huyu pia hapewi udhuru hata kama ataogopa. Hawezi kufanya au kusema neno la kufuru, kama kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah, kumuomba asiyekuwa Allaah, akaitukana Uislamu na waislamu kwa ajili ya kuwaogopa makafiri, akaacha kitu katika mambo ya dini yake kwa sababu ya kuwaogopa makafiri. Amesema (Ta´ala):

وَدُّوا لَوْ تُدْهِنُ فَيُدْهِنُونَ

”Wanatamani lau kama ungelilainisha, nao pia walainishe.” (al-Qalam 68:09)

أَفَبِهَـٰذَا الْحَدِيثِ أَنتُم مُّدْهِنُونَ

”Je, kwa hadithi hii nyinyi ni wenye kuibeza?” (al-Waaqi´ah 56:81)

وَلَوْلَا أَن ثَبَّتْنَاكَ لَقَدْ كِدتَّ تَرْكَنُ إِلَيْهِمْ شَيْئًا قَلِيلًإ

“Na lau kama hakukufanya imara, basi hakika ungelikaribia kuelemea kwao kidogo.” (al-Israa´ 17:73-75)

Mudaahanah haijuzu katika dini ya Allaah hata kama mtu anaogopa. Ni wajibu kwake kushikamana na dini yake hata kama anaogopa midhali hajafikia kiwango cha kutenzwa nguvu. Ikifikia kiwango cha kutenzwa nguvu, basi hapo inajuzu kwake kuwapa kitu katika yale waliyomuomba ili ajiepushe na madhara yao kwa sharti moyo wake utue juu ya imani. Amesema (Ta´ala):

إِلَّا أَن تَتَّقُوا مِنْهُمْ تُقَاةً

”Isipokuwa mkiwa mnajilinda na shari zao.” (Aal ´Imraan 03: 28)

إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا

”… isipokuwa yule aliyelazimishwa na huku moyo wake ukawa umetua juu ya imani. Lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake…” (an-Nahl 16:106)

Ni lazima yapatikane masharti yafuatayo:

1- Shari ya kwanza: Awe ametenzwa nguvu. Si kuogopa peke yake wala kwa sababu ya kutaka kuwapaka mafuta makafiri ili aweze kufikia cheo au manufaa fulani. Asiwapake mafuta katika dini ya Allaah.

2- Sharti ya pili: Moyo wake utue juu ya imani. Atamke kwa ulimi wake tu na wakati huohuo imani yake ibaki ndani ya moyo wake.

3- Sharti ya tatu: Makusudio iwe ni kujikinga na madhara tu na isiwe kwa ajili ya kutaka kuwaridhisha makafiri. Bali makusudio yake iwe ni kujiepusha na madhara yao tu. Kama ilivyokuwa kwa ´Ammaar bin Yaasir (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ndiye sababu ya kuteremka Aayah hii. Makafiri walimchukua na wakamlazimisha kumtukana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hawakumwacha mpaka alipomtukana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akaja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hali ya kuwa ni mwenye kujuta. Akamuuliza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Unahisi vipi moyo wako?” Akasema: “Umetua juu ya imani.”

Ndipo Allaah akateremsha Aayah ifuatayo:

مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اسْتَحَبُّوا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا عَلَى الْآخِرَةِ وَأَنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِين

”Atakayemkufuru Allaah baada ya kuamini kwake [atachukuliwa hatua] – isipokuwa yule aliyelazimishwa na huku moyo wake ukawa umetua juu ya imani. Lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake, basi hao watapata ghadhabu kutoka kwa Allaah na watapata adhabu kubwa. Hivyo kwa sababu wao wamefadhilisha maisha ya dunia kuliko ya Aakhirah na kwamba Allaah hawaongoi watu makafiri.” (an-Nahl 16:106)

Mwenye kuacha kitu katika dini yake kwa ajili ya tamaa ya kidunia au kwa sababu ya kutaka kuwaridhisha makafiri au kwa ajili ya kutaka kuwapaka mafuta, basi anakuwa ni mwenye kufanya kuacha jambo katika dini ya Allaah (´Azza wa Jall) tofauti na kule kuogopa ambako mtu analazimika nako kwa sababu ya kuepuka madhara yao. Ikiwa atasubiri na asichukue ruhusa alopewa, kama alivofanya Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) katika mtihani kuhusu kuumbwa kwa Qur-aan, ndio bora zaidi kuliko kuchukua ruhusa.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 199-201
  • Imechapishwa: 19/03/2019