157. Dalili ya ulazima wa kujitenga mbali na Twaaghuut


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ ۖ قَد تَّبَيَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَيِّ ۚ فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَا انفِصَامَ لَهَا ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

“Hapana kulazimisha katika dini, kwani imekwishabainika kati ya Uongofu na upotofu. Basi atakayemkanusha twaaghuut na akamwamini Allaah kwa hakika atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika, na Allaah ni Mwenye kusikia, Mjuzi wa yote.”[1]

MAELEZO

Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ ۖ قَد تَّبَيَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَيِّ ۚ فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَا انفِصَامَ لَهَا ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

“Hapana kulazimisha katika dini, kwani imekwishabainika kati ya uongofu na upotofu. Basi atakayemkanusha twaaghuut na akamwamini Allaah kwa hakika atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika, na Allaah ni Mwenye kusikia, Mjuzi wa yote.”[2]

Hakuna kulazimisha katika dini maana yake ni kwamba haifai kumlazimisha yeyote kuingia ndani ya Uislamu. Kwa sababu kuingia ndani ya Uislamu ni lazima iwe kwa kukinaika, kuamini moyoni na asilazimishwe yeyote. Ni jambo haliyumkiniki. Kwa sababu hakuna awezaye kuziendesha nyoyo isipokuwa Allaah. Halazimishwi yeyote kuingia katika Uislamu kwa sababu sisi hatuzimiliki nyoyo. Allaah (Jalla wa ´Alaa) ndiye mwenye kuzimiliki na kuziendesha. Lakini sisi jukumu letu ni kulingania katika Uislamu na kuuvutia. Tunapambana katika njia ya Allaah kwa yule mwenye kukufuru kwa sababu ya kuueneza Uislamu na kumpa fursa anayetaka kusilimu. Sababu nyingine ni kuwakandamiza maadui wa Allaah. Kuhusu uongofu uko mikononi mwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hakuna yeyote anayelazimishwa juu ya Uislamu na imani. Hiki ni kitu kinachorejea kwake mwenyewe. Amesema (Ta´ala):

قَد تَّبَيَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَيِّ

”Kwani imekwishabainika kati ya uongofu na upotofu.”

Hakuna kinachochukiza ndani ya Uislamu. Bali yote yaliyomo ndani ni yenye kupendwa. Kufuru na shirki yote ni shari na yenye kuchukiwa. Kila kitu kimepambanuka na kingine. Uongofu ambao ni haki umepambanuka kutokamana na upotofu ambao ni batili. Mtu yuko na akili na yuko na fikira na uzani ambapo anaweza kupima kati ya haki na batili. Fikira yake ikiwa imesalimika kutokamana na matamanio basi itampelekea katika kuikubali haki pasi na kuichukia. Haya ni moja ya maoni kuhusu Aayah.

Maoni ya pili yanasema kuwa Aayah imeteremka juu ya Ahl-ul-Kitaab na kwamba Ahl-ul-Kitaab hawalazimishwi kuingia ndani ya Uislamu. Bali wakitaka kubaki juu ya dini yao wanaruhusiwa wanaweza kufanya hivo kwa sharti walipe kodi kuwapa waislamu wakiwa ni wenye kunyenyekea. Ama makafiri wengine haikubaliwi kutoka kwao usiokuwa Uislamu au kuuliwa. Kwa sababu hawana dini. Uabudiaji masanamu ni dini batili.

Maoni ya tatu ni kwamba Aayah hii imefutwa kwa Aayah ya Jihaad. Hapa ilikuwa mwanzoni mwa Uislamu kabla ya kuwekwa Shari´ah ya Uislamu. Baadaye kulipowekwa Shari´ah ya Uislamu Aayah hii ikafutwa.

Lakini maoni ya kwanza ndio sahihi kwamba Aayah haikufutwa na kwamba dini haingii ndani ya mioyo kwa kulazimisha bali mtu anaingia kwa kutaka kwake mwenyewe. Lakini asiyekubali dini anataamiliwa matangamano yanayoendana naye ima kuuliwa au kuchukua kodi kwa yule ambaye Allaah amesunisha juu yake.

فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ

”Basi atakayemkanusha twaaghuut na akamwamini Allaah… ”

Makusudio ya Twaaghuut ni Twawaaghiyt wote katika ´ibaadah, katika kufuata au katika kutii. Kwa sababu neno hilo hapa limekuja kwa kuenea. Ametanguliza kukufuru Twaaghuut kabla ya kumwamini Allaah kwa sababu kumwamini Allaah hakunufaishi isipokuwa baada ya kukufuru Twaaghuut. Yule mwenye kumwamini Allaah na asikufuru Twaaghuut basi haitomfaa kitu imani yake. Ambaye anajiita ni muumini, anaswali, anafunga, anatoa zakaah na anafanya matendo mema lakini hata hivyo hajitengi mbali na shirki wala washirikina na anasema kuwa yeye hana chochote kuhusiana na wao, mtu huyu anazingatiwa sio muislamu kwa sababu hakukufuru Twaaghuut. Ni lazima kukufuru Twaaghuut ikiwa na maana ya kuikataa Twaaghuut na kuamini ubatilifu wake na kujiweka mbali nayo na watu wake. Ni lazima kupatikane jambo hilo. Imani haisihi isipokuwa baada ya kukufuru Twaaghuut. Katika Aayah nyingine imekuja:

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

”Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut [waungu batili].”[3]

´Ibaadah ya kumwabudu Allaah haisihi isipokuwa baada ya kujitenga mbali na Twaaghuut. Vinyume viwili havikusanyiki. Imani na ukafiri havikusanyiki moyoni. Imani na kufuru kubwa havikusanyiki moyoni. Kuhusu kufuru ndogo vinaweza kukusanyika.

[1] 02:256

[2] 02:256

[3] 16:36

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 306-309
  • Imechapishwa: 25/02/2021