156. Hakuna tofauti kati mwenye kufanya mzaha, anayekusudia au mwenye kuogopa

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Na wala hakuna tofauti katika vichenguzi hivi Uislamu kati ya mwenye kufanya mzaha na mwenye kukusudia na mwenye kuogopa isipokuwa tu yule aliyetenzwa nguvu…

MAELEZO

Hakuna tofauti katika vichenguzi vyote hivi.

Mwenye kufanya mzaha ni yule ambaye anasema maneno ya kuritadi hali ya kufanya utani.

Mwenye kukusudia ni yule ambaye anakusudia akisemacho.

Dalili ya hayo ni kile kisa ambacho Allaah kakitaja katika Qur-aan wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa anatoka katika vita vya Tabuuk ambapo wakakaa na kupiga soga. Mmoja wao akasema:

“Hatujapata kuona watu kama wasomaji wetu hawa; matumbo yao yanapenda kula sana, ndimi zao zinasema uongo sana na ni waoga wakati wa mapambano – yaani anamkusudia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake. Katika majlisi hiyo kulikuwepo kijana ambaye anaitwa ´Awf bin Maalik, akamkema na kumwambia: “Umesema uongo, lakini wewe ni mnafiki. Nitamweleza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Akaenda ili kumweleza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akakuta Wahy umeshamtangulia na kuteremka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu khabari za watu hawa.  Wakaja kutoa udhuru juu ya waliyoyasema na wakasema:

“Ee Mtume wa Allaah! Hakika sisi tulikuwa tukiongea tu ili kufupisha urefu wa safari. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hamtazami na huku ameshikilia kamba za ngamia wake. Mtume hamtazami na hakuna anachozidisha zaidi ya kusoma Aayah ifuatayo:

وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ ۚ قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Ukiwauliza, basi bila shaka watasema: “Hakika sisi tulikuwa tunaporoja na tunacheza.” Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?”  Msitoe udhuru; mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.” (at-Tawbah 09:65-66)

pamoja na kwamba walitoa udhuru kwamba eti walikuwa wakifanya mzaha tu. Hata hivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hakuwapa udhuru. Hakuna tofauti kati ya mwenye kukusudia kweli na mwenye kufanya mzaha.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 197-199
  • Imechapishwa: 19/03/2019