Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Twawaaghiyt ni wengi. Wakubwa wao ni watano:

1- Ibliys, Allaah amlaani.

MAELEZO

Twawaaghiyt ni wengi… – Twawaaghiyt ambao wanaendana na maana hii  “kila chenye kuabudiwa, kinachofuatwa au kutiiwa ambacho mja anapindukia mipaka yake.” Lakini viongozi na wakuu wao ni watano:

1- Ibliys, Allaah amlaani – Bi maana ambaye amefukuzwa na kuwekwa mbali na rehema za Allaah kwa sababu alikataa kumsujudia Aadam na akamuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), akafanya kiburi na akasema:

قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ ۖ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ

”Akasema: ”Mimi ni bora kuliko yeye; umeniumba kutokana na moto naye umemuumba kutokana na udongo.”[1]

Akaasi amri na kufanya jeuri ambapo Allaah akamlaani, akamtukuza, akamtenga mbali na akaitwa ”Ibliys” kwa sababu amekatishwa (أبلس) tamaa na huruma ya Allaah. Ibliys ni yule aliyekata tamaa ya kitu. Ibliys, aliyelaaniwa na Allaah, ndiye kiongozi wa Twaaghuut kwa sababu yeye ndiye huamrisha kuabudiwa mwengine asiyekuwa Allaah, pia yeye ndiye huamrisha kumfuata mwingine asiyekuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yeye ndiye huamrisha kumtii asiyekuwa Allaah katika kuhalalisha na kuharamisha. Ibliys ndiye chanzo cha shari na ndiye kiongozi wa Twawaaghiyt.

[1] 38:76

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 230
  • Imechapishwa: 23/02/2021