153. Kukaa masiku kadhaa kwa ajili ya kumsomea Qur-aan maiti


Swali 153: Sisi huku kwetu Syria kuna mila mbalimbali na chache ambazo wakati mwingine zinastaajabisha kutokana na yale yaliyoko kwa wengine. Kwa mfano tunapofiwa na maiti basi watu huharakia kutoa rambirambi hali ya kuwa ni wenye kubeba kile chakula wanachoweza ikiwa ni pamoja na sukari, mchele na vyenginevyo kwa muda usiyopungua wiki moja. Wanaketi na wanabadilishana mazungumzo, wanakunywa chai na sigara na khaswa hookah[1] na wanarefusha vikao vyao. Baada ya alasiri kila siku wanasoma kile kinachoitwa “khitmah”. Kila mtu anasoma juzu yake ya Qur-aan kisha kunatimia zawadi yake kwa maiti. Wakati mwingine tunawaona watu wawili wanasoma juzu moja. Mmoja anasoma kurasa moja na mwengine anaendelea na kurasa ya pili ili waharakishe kusoma juzu.  Hufanywa vivo hivyo siku ya arobaini. Kwa sababu hayo hukamilika baada ya swalah ya Dhuhr na kunatolewa karamu moja au karamu mbili katika chakula cha mchana. Una maoni gani juu ya hayo[2]?

Jibu: Ni jambo limewekwa katika Shari´ah kuwapa mkono wa pole wafiwa wa maiti. Vivyo hivyo kuwatumia chakula. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaamrisha familia yake kuwatengenezea familia ya Ja´far bin Abiy Twaalib chakula wakati alipofikiwa na khabari ya kifo chake na akasema:

“Kwani hakika wamefikwa na kitu kinachowashughulisha.”[3]

Kuhusu familia ya maiti au watu wengine kukaa siku moja au zaidi kwa ajili ya kusoma Qur-aan na kumpa zawadi maiti ni jambo la Bid´ah na halina msingi katika Shari´ah takasifu. Vivyo hivyo yale mliyotaja yanayofanywa katika siku ya arobaini hayana msingi katika Shari´ah.

Kuhusu uvutaji wa sigara ni dhambi katika nyakati zote na madhara yake ni mengi.

Tunamwomba Allaah awalinde waislamu kutokamana na shari yake na shari nyenginezo zote na awawafikishe kufuata Sunnah na kutahadhari katika mambo yao yote. Kwani hakika Yeye ni Mwingi wa kutoa, Mkarimu.

[1] Tazama https://en.wikipedia.org/wiki/Hookah

[2] Majmuu´-ul-Fataawaa (13/396-397).

[3] Ahmad (1754), Ibn Maajah (1610), at-Tirmidhiy (998) na Abu Daawuud (3132).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz, uk. 112-113
  • Imechapishwa: 25/01/2022