152. Watu watatu wataotupwa Motoni siku ya Qiyaamah

Malengo ya kujifunza elimu ni kwa ajili ya kuifanyia kazi. Mtu hajifunzi elimu ili ajue tu, aambiwe kuwa ni ´mwanachuo` au asifiwe na wala malengo yake sio matendo. Isipokuwa alichokusudia ni ili ajue tu, asifiwe, cheo chake kiinuke mbele ya watu, yule ambaye hii ndio hamu na malengo yake basi atakuwa miongoni mwa watu wa mwanzo watakaowekwa Motoni siku ya Qiyaamah. Watu wa kwanza ambao wataingizwa Motoni siku ya Qiyaamah ni watu aina tatu; mpigana jihaad, mtoa swadaqah na mwanachuoni[1].

Mpigana jihaad ambaye alipigana jihaad mpaka akauawa. Atakuja siku ya Qiyaamah na Allaah atamwambia: “Ulifanya nini?” Aseme: “Ee Mola Wangu! Nilipigana jihaad kwa ajili Yako mpaka nikauawa.” Ataambiwa: “Umesema uongo, ulipigana ili uambiwe kuwa ni shujaa na kumeshasemwa. Kisha atatupwa Motoni.

Kisha ataletwa mtoaji swadaqah na kuambiwa: “Ulifanya nini?” Atasema: “Sikuacha njia yoyote ambayo inahitajia kutolewe isipokuwa nilitoa kwa ajili Yako.” Allaah atamwambia: “Umesema uongo, ulitoa swadaqah ili uambiwe ni mtoaji sana na kumeshasemwa. Kisha atatupwa Motoni.

Kisha ataletwa mwanachuonina Allaah atamwambia: “Ulifanya nini?” Atasama: “Ee Allaah! Nilijifunza elimu kwa ajili Yako na nikaifunza.” Allaah atamwambia: “Umesema uongo, ulijifunza ili uambiwe kuwa wewe ni mwanachuoni na kumeshasemwa. Halafu atatupwa Motoni.

Hawa ndio wataanza kutupwa Motoni kabla ya waabudu masanamu. Watasema: “Ee Mola wetu! Vipi tutaadhibiwa kabla ya waabudu masanamu?” Allaah (Jalla wa ´Alaa) atajibu: “Yule mwenye kujua si sawa na yule asiyejua.” Maneno haya ni muhimu sana; jambo la kujifunza na la kuifanyia kazi hio elimu kwa matendo. Mwenye kuyakataa au akakataa kimoja wapo, basi anaritadi kutoka katika dini ya Uislamu.

[1] Shaykh (Hafidhwahu Allaah) anaashiria  Hadiyth ambayo ameipokea Muslim kwa nambari. (1905), at-Tirmidhiy (2382), an-Nasaa´iy (3137) na Ahmad (8277).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 191-193
  • Imechapishwa: 14/03/2019