152. Shirki ya utiifu


Hakuna njia ya kumfikia Allaah (Jalla wa ´Alaa) isipokuwa kwa kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Ta´ala):

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ ۖ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْكَافِرِينَ

“Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi. Hivyo atakupendeni Allaah na atakusameheni dhambi zenu na Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.” Sema: “Mtiini Allaah na Mtume, mkikengeuka basi hakika Allaah hawapendi makafiri.[1]

Ambaye anamfuata asiyekuwa Mtume huyu anazingatiwa ni Twaaghuut. Vivyo hivyo yule anayewaita watu kumfuata na kuwaambia watu kwamba yeye atawaletea mambo moja kwa moja kutoka kwa Allaah, huyu ni Twaaghuut mkubwa ulimwenguni.

Maneno yake:

”… au chenye kutiiwa… ”

Mwenye haki ya kutiiwa ni Allaah na Mtume Wake katika yale waliyohalalisha na wakaharamisha. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi; mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[2]

Halali ni ile iliyofanywa na Allaah kuwa halali na haramu ni ile iliyofanywa na Allaah kuwa haramu. Haifai kwa yeyoye kushirikiana na Allaah katika kuhalalisha na kuharamisha. Kadhalika ndio maana Allaah amemhukumu kuwa ni mshirikina yule anayehalalisha au akarahamisha au akamtii mwenye kufanya hivo. Amesema (Ta´ala):

فَكُلُوا مِمَّا ذُكِرَ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ إِن كُنتُم بِآيَاتِهِ مُؤْمِنِينَ وَمَا لَكُمْ أَلَّا تَأْكُلُوا مِمَّا ذُكِرَ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ وَقَدْ فَصَّلَ لَكُم مَّا حَرَّمَ عَلَيْكُمْ إِلَّا مَا اضْطُرِرْتُمْ إِلَيْهِ ۗ وَإِنَّ كَثِيرًا لَّيُضِلُّونَ بِأَهْوَائِهِم بِغَيْرِ عِلْمٍ ۗ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِالْمُعْتَدِينَ وَذَرُوا ظَاهِرَ الْإِثْمِ وَبَاطِنَهُ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَكْسِبُونَ الْإِثْمَ سَيُجْزَوْنَ بِمَا كَانُوا يَقْتَرِفُونَ وَلَا تَأْكُلُوا مِمَّا لَمْ يُذْكَرِ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ وَإِنَّهُ لَفِسْقٌ ۗ وَإِنَّ الشَّيَاطِينَ لَيُوحُونَ إِلَىٰ أَوْلِيَائِهِمْ لِيُجَادِلُوكُمْ ۖ وَإِنْ أَطَعْتُمُوهُمْ إِنَّكُمْ لَمُشْرِكُونَ

”Basi kuleni katika ambavyo vimetajiwa jina la Allaah [wakati wa kuchinjwa kwake] mkiwa nyinyi ni wenye kuziamini Aayah Zake. Na mna nini hata msile katika ambavyo ambavyo vimetajiwa jina la Allaah na ilhali amekwishakupambanulieni yale aliyokuharamishieni isipokuwa vile mlivyofikwa na dharura navyo. Na hakika wengi wanawapotosha [wenzao] kwa matamanio yao pasi na elimu. Hakika Mola wako Yeye anajua Zaidi wenye kuchupa mpaka. Na acheni dhambi za waziwazi na zilizofichika. Hakika wale wanaochuma dhambi basi watalipwa kwa yale waliyokuwa wakiyachuma. Na wala msile katika ambavyo havikutajiwa jina la Allaah [katika kuchinjwa kwake], kwani huo ni ufasiki. Na hakika mashaytwaan wanadokeza wapenzi wao wabishane nanyi; na mtakapowatii basi hakika mtakuwa washirikina.”[3]

Kwa sababu watu wa kipindi cha kikafiri walikuwa wakisema kuwa nyamafu ni halali kwa sababu Allaah ndiye kamchinja. Wakawa wanasema kuwa nyamafu ana haki zaidi ya uhalali kuliko vile walivyochinja wengine. Allaah amesema kuwa watu wasile isipokuwa kile kilichochinjwa kwa mujibu wa Shari´ah na amekuharamishieni wanyama waliokufa wenyewe. Upande wa pili watu hawa wakasema kuwa nyamafu ni halali na kwamba ndio yenye haki zaidi ya kuwa halali kuliko vile vilivyochinjwa. Kwa sababu vichinjwa vimechinjwa na watu wenyewe na kwamba nyamafu Allaah ndiye kaichinja. Ndio maana akawaraddi washirikina na akasema:

وَلَا تَأْكُلُوا مِمَّا لَمْ يُذْكَرِ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ وَإِنَّهُ لَفِسْقٌ

”Na wala msile katika ambavyo havikutajiwa jina la Allaah [katika kuchinjwa kwake], kwani huo ni ufasiki.”

Bi maana ni kutoka nje ya kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Akasema baada yake:

وَإِنَّ الشَّيَاطِينَ لَيُوحُونَ إِلَىٰ أَوْلِيَائِهِمْ

”Na hakika mashaytwaan wanadokeza wapenzi wao.”

Wanasema kuwa nyamafu amechinjwa na Allaah na vichinjwa vimechinjwa na wao wenyewe na kwamba ni vipi wanahalalisha vile walivyochinja wao na kwamba hawahalalishi kile kilichochinjwa na Allaah? Huu ni ubishi wa batili. Kisha akasema (Ta´ala):

وَإِنْ أَطَعْتُمُوهُمْ إِنَّكُمْ لَمُشْرِكُونَ

”Mtakapowatii basi hakika mtakuwa washirikina.”[4]

Hii ni shirki ya utiifu. Kuhalalisha na kuharamisha ni haki ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Kwa hiyo haijuzu kwa yeyote kuhalalisha au kuharamisha kutoka kichwani mwake au akamtii mwenye kuhalalisha au kuharamisha kutoka kichwani mwake yeye. Yule mwenye kufanya hivo ni Twaaghuut na mwenye kuwatii Twawaaghiyt ambao wanahalalisha na  wanaharamisha badala ya Allaah. Hii ndio maana ya:

”… au chenye kutiiwa… ”

Bi maana mwenye kutii katika kuhalalisha na kuharamisha. Kwa sababu kuhalalisha na kuharamisha ni haki ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye mwenye kufikisha kutoka kwa Allaah yale aliyohalalisha na kuharamisha.

[1] 03:31-32

[2] 04:59

[3] 06:118-121

[4] 06:118-121

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 298-300
  • Imechapishwa: 23/02/2021