151. Mambo ya arobaini na miaka hayana msingi katika Shari´ah


Swali 151: Ni ipi hukumu ya mila mbalimbali zinazofanywa wakati wa tanzia;  kufanya chakula, kusoma Qur-aan, mambo ya arobaini, mambo ya miaka na mfano wake[1]?

Jibu: Desturi hizi hazina msingi katika Shari´ah takatifu na hazina msingi wowote. Bali ni miongoni mwa Bid´ah na ni miongoni mwa mambo ya kipindi cha kikafiri. Anapokufa maiti kukafanywa karamu ambapo wakaalikwa majirani, jamaa na wengineo kwa ajili ya kutoa rambirambi ni Bid´ah na haijuzu. Vivyo hivyo kufanya mambo haya kila wiki au mwanzoni mwa mwaka mpya yote ni katika Bid´ah za kipindi cha kikafiri. Kilichowekwa katika Shari´ah kwa wafiwa wa maiti ni kuvuta subira na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah na kusema kama wanavosema wenye kusubiri:

إنا لله وإنا إليه راجعون

“Hakika sisi ni wa Allaah na hakika Kwake tutarejea.”

Allaah amewaahidi kheri nyingi. Amesema (Subhaanah):

أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Hao zitakuwa juu yao sifa kutoka kwa Mola wao na rehema; na hao ndio wenye kuongoka.”[2]

Hapana vibaya kwao kujitengenezea chakula kama kawaida kwa ajili ya kula na mahitaji yao. Vivyo hivyo wakipata wageni ni sawa wakawatengenezea chakula kinachonasibiana nao. Hilo ni kutokana na ueneaji wa dalili juu yake.

Imesuniwa kwa jamaa na majirani kuwatengeneza chakula na wakawaagizia nacho. Kwa sababu imethibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofikiwa na khabari za kufa kwa Ja´far bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) wakati alipouliwa katika Mu´tah huko Shaam alisema kuiambia familia yake:

“Watengenezeeni familia ya Ja´far chakula. Kwani hakika wamefikwa na kitu kinachowashughulisha.”[3]

Kwa hiyo ikafahamisha kwamba imesuniwa kuwatumia chakula wafiwa wa maiti kitachotoka kwa jamaa au wengineo katika yale masiku ya msiba.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (13/394-395).

[2] 02:157

[3] Ahmad (1754), Ibn Maajah (1610), at-Tirmidhiy (998) na Abu Daawuud (3132).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz, uk. 109-110
  • Imechapishwa: 24/01/2022