15. Zakaat-ul-Fitwr


Zakaat-ul-Fitwr ni faradhi kwa kila muislamu, mdogo na mkubwa, mwanaume na mwanamke, aliye huru na mtumwa. Imethibiti kuwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifaradhisha Zakaat-ul-Fitwr Swaa´ moja ya tende au Swaa´ moja ya shayiri kwa waislamu wanaume na wanawake, wadogo na wakubwa, walio huru na watumwa na ameamrisha itolewe kabla ya watu hawajatoka kuswali.”[1]

Hakuna kiwango maalum cha mali anachotakiwa mtu kumiliki ili iwe wajibu kutoa Zakaat-ul-Fitwr. Maadamu muislamu na familia yake wana chakula cha kutosha mchana na usiku basi ni wajibu kujitolea yeye mwenyewe, wanawe, wakeze na watumwa wake.

Kuhusu mfanya kazi aliyekodeshwa, anatakiwa kujilipia mwenyewe isipokuwa ikiwa kama bosi wake atamlipia kwa kupenda kwake mwenyewe au akamshurutishia hilo. Ama mfanya kazi ambaye ni mtumwa, bosi wake ndiye anatakiwia kumlipia.

Sio wajibu kumtolea Zakaat-ul-Fitwr mtoto aliye tumboni kwa maafikiano. Lakini imependekezwa kutokana na kitendo cha ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh).

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba amesema:

“Wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tulikuwa tukiitoa Swaa´ moja ya chakula, tende, shayiri, jibini au zabibu.”[2]

Kuna kundi la wanachuoni wamefasiri kuwa ni nafaka na wengine wakafasiri kuwa ni chakula kinacholiwa katika mji sawa iwe ni nafaka, mahindi, mtama au kitu kingine. Maoni haya ndio ya sawa kwa sababu zakaah ni matajiri kuwatazama vizuri mafakiri. Hata hivyo sio wajibu kwa muislamu kufanya kitu kingine kisichokuwa chakula kinacholiwa ndani ya mji wake.

Kiwango cha wajibu ni Swaa´ ya kinabii. Swaa´ ya kinabii ni sawa na takriban 3 kg zilizochujwa. Allaah (Subhaanah) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا كَسَبْتُمْ

“Enyi mlioamini! Toeni katika vizuri mlivyochuma.”[3]

Hilo linatakasa zaidi dhamiri na ni kumfanyia vizuri fakiri. Isipokuwa tu shayiri sio wajibu kuichuja kutokana na usumbufu unaopatikana kwa kufanya hivo. Mchele au kitu kingine katika nafaka ambacho bora ni kukitoa bila ya kukichuja kwa njia ya kwamba kitakuwa sawa na kile kiwango cha nafaka ambacho kimechujwa, ni sawa – Allaah akitaka – kwa kuzingatia manufaa ya mmiliki na fakiri.

Lililo bora ni kutoa Zakaat-ul-Fitwr kuwapa mafukara wa mji asubuhi ya siku ya ´Iyd. Inatakiwa kutolewa kabla ya swalah. Inajuzu kuitoa siku moja au mbili kabla ya haijagawiwa tarehe 28. Mtu akisafiri siku mbili kabla ya siku ya ´Iyd atatoa Zakaat-ul-Fitwr katika nchi ya Kiislamu aliyofika. Nchi ikiwa sio ya Kiislamu atafute mafakiri wa Kiislamu waliyoko katika nchi  hiyo na awape. Ikiwa mtu safari yake itakuwa baada ya kujuzu kutoa Zakaat-ul-Fitwr, imewekwa katika Shari´ah aitoe kuwapa mafukara wa mji wake. Malengo yake ni kuwaangalia, kuwatendea wema na kuwatajirisha kutokamana na watu katika yale masiku ya ´Iyd.

Imethibiti kwamba Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemfaradhishia Zakaat-ul-Fitwr mfungaji ili imtwaharishe kutokamana na upuuzi na ugomvi na kuwalisha masikini. Atayeitoa kabla ya swalah basi hiyo ni zakaah yenye kukubaliwa na atayeitoa baada ya swalah ni swadaqah miongoni mwa swadaqah  zengine.”[4]

Wanachuoni wengi wanaonelea kuwa Zakaat-ul-Fitwr haijuzu kutoa pesa. Maoni haya ndio sahihi zaidi. Ni wajibu kutoa Zakaat-ul-Fitwr katika chakula. Hivyo ndivyo alivyofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake na ndio maoni yaliyo na wanachuoni wengi.

Ninamuomba Allaah atuwafikishe sisi na waislamu wengine wote kuwa na uelewa katika dini na msimamo juu yake na azitengeneze nyoyo na matendo yetu. Hakika Yeye ni Mwingi wa kutoa na mkarimu.

Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake.

[1] al-Bukhaariy (1503) na Muslim (984).

[2] al-Bukhaariy (1508) na Muslim (985).

[3] 02:267

[4] Abu Daawuud (1609) na ad-Daaraqutwniy (2/138). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Abiy Daawuud” (1420).