Swali 15: Baadhi ya watu wanasema kuwa miezi yote haifahamiki kuanza na kumalizika kwake kwa kuonekana mwezi mwandamo. Kwa mfano kukamilisha idadi ya siku thelathini Sha´baan na vivyo hivyo Ramadhaan. Ni ipi hukumu ya Shari´ah kwa maneno kama haya?

Jibu: Maneno haya kwa upande fulani kwamba miezi yote haifahamiki kuanza na kuisha kwake kwa kuonekana mwezi mwandamo si kweli. Bali kuona mwezi mwandamo juu ya miezi yote ni jambo linalowezekana. Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mkiuona, basi fungeni, na mkiuona fungueni.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hafungamanshi hukumu juu ya jambo ambalo ni muhali. Na ikiwa inawezekana kuona mwezi mwandamo wa Ramadhaan basi ni jambo linalowezekana kuona mwezi mwandamo juu ya miezi mingine.

Kuhusu kipengele cha pili cha swali kwamba kinachotakikana ni kukamilisha idadi ya siku thelathini za Sha´baan na vivyo hivyo idadi ya siku za Ramadhaan. Sahihi ni kwamba tukifunikwa na wingu na tusione mwezi mwandamo, bali umejificha kwa wingu na mfano wake, basi tutatakiwa kukamilisha idadi ya Sha´baan siku thelathini kisha tuanze kufunga. Pia tukamilishe idadi ya Ramadhaan siku thelathini kisha tufungue. Namna hii ndivo zilivyopokelewa Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Fungeni mtakapouona na fungueni mtakapouona. Mkifunikwa na wingu basi hesabuni siku thelathini.”

Katika Hadiyth nyingine imekuja:

”…  kamilisheni idadi ya siku thelathini.”[2]

Kutokana na haya ikiwa ni usiku wa kuamkia tarehe thelathini Sha´baan na watu wakautafuta mwezi mwandamo lakini wasiuone, basi watakamilisha Sha´baan siku thelathini. Na ikiwa ni usiku wa tarehe thelathini Ramadhaan na watu wakautafuta mwezi mwandamo lakini wasiuone, basi watakamilisha idadi ya Ramadhaan siku thelathini.

[1] al-Bukhaariy (1900) na Muslim (2471).

[2] al-Bukhaariy (1909) na Muslim (2481).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 48 mas-alatu fiy Swiyaam, uk. 17-18
  • Imechapishwa: 15/04/2021