15. Ubainifu wa ni nani walii wa Allaah na asiyekuwa yeye

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Msingi wa tano:

Kubainisha kwa Allaah (Subhaanah) mawalii wa Allaah na kutofautisha baina yao na wale wenye kujifananisha na wao miongoni mwa maadui wa Allaah katika wanafiki na watu waovu. Inatosha katika hili Aayah moja katika Suurah ”Aal ´Imraan” ambayo ni maneno Yake:

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ

“Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni atakupendeni Allaah.”[1]

Na Aayah katika Suurah “al-Maaidah” ambayo ni maneno Yake:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا مَن يَرْتَدَّ مِنكُمْ عَن دِينِهِ فَسَوْفَ يَأْتِي اللَّـهُ بِقَوْمٍ يُحِبُّهُمْ وَيُحِبُّونَهُ

“Enyi mlioamini! Yeyote atakayeritadi miongoni mwenu kutoka dini yake, basi punde tu Allaah ataleta watu [badala yao] atakaowapenda nao watampenda.” (05:54)

”Aayah nyingine katika Suurah “Yuusuf” ambayo ni maneno Yake:

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ

“Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hawana khofu juu yao na wala hawatohuzunika. Ambao wameamini na wakawa na uchaji.” (10:62-63)

Kisha mambo yakawa kwa wengi wenye kudai elimu na kwamba yeye ni katika waongofu wa viumbe na wenye kuilinda Shari´ah juu ya kwamba mawalii ni lazima kwao kutowafuata Mitume, na yule mwenye kuwafuata [Mitume] sio katika wao [mawalii]. Isitoshe ni lazima kuacha Jihaad, na yule mwenye kupigana Jihaad sio katika wao [mawalii]. Vilevile ni lazima kuacha imani na kumcha Allaah, na yule mwenye kushikamana na imani na kumcha Allaah basi si katika wao [mawalii hao]. Ee Mola Wetu! Tunakuomba msamaha na afya. Hakika Wewe ni mwingi wa kusikia du´aa.

MAELEZO

Kubainisha kwa Allaah (Subhaanah) mawalii wa Allaah… – Mawalii wa Allaah ni wale walioamini na wakamcha na wakanyooka juu ya dini Yake. Ni wale ambao Allaah amewasifu pale aliposema (Subhaanahu wa Ta´ala):

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ

“Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hawana khofu juu yao na wala hawatohuzunika. Ambao wameamini na wakawa wanamcha.”

Si kila ambaye anadai uwalii anakuwa walii. Vinginevyo kila mmoja angekuwa anaudai. Huyu mwenye kudai uwalii atapimwa kutokana na matendo yake; ikiwa matendo yake yamejengeka juu ya imani na kumcha Allaah basi kweli atakuwa ni walii wa Allaah. Viginevyo sio walii wa Allaah. Isitoshe kitendo cha kudai uwalii ni kujitakasa nafsi na ni jambo linapingana na kumcha Allaah. Kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

فَلَا تُزَكُّوا أَنفُسَكُمْ ۖ هُوَ أَعْلَمُ بِمَنِ اتَّقَىٰ

“Hivyo basi msizitakase nafsi zenu. Yeye anamjua zaidi ni nani mwenye kumcha Allaah.”[2]

Mtu akidai kuwa yeye ni katika mawalii wa Allaah basi ameitakasa nafsi yake. Basi hapo anakuwa ametumbukia katika kumuasi Allaah na jambo ambalo Allaah amemkatalia, kitu ambacho kinapingana na kumcha Allaah. Mawalii wa Allaah hawazitakasi nafsi zao kwa ushuhuda kama huu. Si vinginevyo wao ni wenye kumwamini Allaah na kumcha na wanamtii (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa njia kamilifu zaidi. Hawawaghuri watu na kuwahadaa kutokana na madai haya mpaka wahakikishe wamewapotosha kutokamana na njia ya Allaah.

Watu hawa ambao wakati fulani hujiita kwamba eti ni mabwana (أسيادًا) na wakati mwingine eti ni mawalii, endapo mtu atazingatia yale wayafanyayo basi atakuta kuwa wako mbali kabisa kutokamana na huyo uwalii na ubwana.

[1] 03:31

[2] 53:32

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 26-27
  • Imechapishwa: 23/06/2021